Mchangani

Ligi ngazi ya Taifa mkoa wa Dodoma kutimua vumbi jan27

Sifa Lubasi, Dodoma

LIGI ya Taifa ngazi ya Mkoa wa Dodoma inatarajiwa kuanza Januari 27 ambapo timu 18 kutoka wilaya zote za Mkoa wa Dodoma zinatarajiwa kushiriki. Ligi hiyo itachezwa katika vituo viwili vya Dodoma Mjini na Kongwa.

Akizungumza na gazeti hili Katibu Mkuu wa Chama Cha Soka Mkoa wa Dodoma (DOREFA) Abubakary Ibrahim alisema tayari semina elekezi imefanywa kwa viongozi na waamuzi na wako mbioni kukamilisha ratiba ya ligi hiyo.

Alizitaja timu zilizopangwa katika kituo cha Kongwa huku sehemu zilizotoka zikiwa kwenye mabano ni Inkata, Cargo (Kongwa), Mpwapwa Stars (Mpwapwa), Kivukoni (Chamwino), The Gunners (Dodoma), Magereza (Isanga Dodoma), Bafana Bafana (Chamwino), Maskani (Bahi) na Bus Stand (Mpwapwa).

Katika kituo cha Dodoma timu zitakazoshiriki ni CDA, Polisi Jamii (Dodoma), Bonde la Ufa (BAHI), City Centre (Kondoa), Chipanga (Bahi), Chinga (Kondoa), Magereza (Mpwapwa), Vijana (Chamwino) na Beach Boys (Kongwa).

Katibu huyo wa DOREFA alisema kuwa timu zitagawanywa katika makundi mawili ambapo kila kundi litatoa timu tatu zitakazoingia kwenye sita bora kabla ya bingwa wa mkoa kupatikana.

Alisema kuwa mwishoni mwa wiki iliyopita kulikuwa na semina elekezi na uchambuzi wa fomu za viongozi wote na kila timu ilileta Kocha na Katibu.

Alitaja mambo yaliyojadiliwa katika semina hiyo kuwa ni utawala wa soka, sheria za soka, sifa za mwalimu bora, kanuni za mashindano, upatikanaji wa timu za usajili.

Aidha alisema kuwa, dosari kadhaa zilijitokeza ambapo fomu nyingi zilikuwa na picha pungufu na kwamba wahusika wametakiwa kurekebisha dosari hizo kabla ya Jumamosi na kila timu kuwasilisha nakala ya usajili wa klabu zao.

“Tutatoa ratiba baada ya fomu zenye makosa kurekebishwa na kurudishwa kwetu tena na timu ambazo tutaona hazijakidhi vigezo tutaziondoa,” alisema.

Wakati huo huo,Timu ya soka ya watoto wenye umri wa miaka 13 imeundwa katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Lengo la kuundwa kwa timu hiyo ni kujaribu kuinua vipaji katika soka la wanawake tangu wakiwa na umri mdogo.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.