TIMU ya taifa ya gofu ikiwa na wachezaji wanne na viongozi wawili
imeondoka jana jioni Dar es Salaam kwenda Kitwe, Zambia kwa ajili ya
mashindano ya Afrika ya President Cup yaliyopangwa kuanza kesho hadi
Oktoba 2, ikiwa na matumaini ya kurejea na kombe.
Wakizungumza Dar es Salaam leo wakati wa hafla ya kukabidhiwa bendera
ya taifa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Dioniz
Malinzi, viongozi, kocha na wachezaji kwa pamoja walisema wamejiandaa
vema kushindana na kurejea na taji.
Malinzi, ambaye pia ndiye mdhamini wa timu alisema ana imani kwamba
wanakwenda kushindana na sio kushiriki. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha
Gofu Tanzania (TGU), Joseph Tango ambaye ndiye mkuu wa msafara alisema
vijana wameandaliwa vema na ari ya timu ipo juu.
“Tumekuwa na karibu wiki mbili za maandalizi kwenye viwanja vya
Gymkhana Dar es Salaam chini ya kocha Mbwana Juma na wachezaji wapo
kwenye hali nzuri,” alisema Tango.
Alimshukuru Malinzi kwa moyo wa kizalendo wa kusaidia michezo na kuomba Watanzania wengine kuiga mfano wake.
Alisema gofu inahitaji wadhamini ili kufanikisha mipango yake mingi
ikiwepo ya kuinua mchezo huo kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu na
pia kushiriki mashindano ya ndani na nje ya nchi ambayo mengi
wameshindwa kwenda kwa kukosa udhamini.
Kocha Juma alisema timu wanayoihofia ni Afrika Kusini pekee kutokana
na ubora wao, lakini kwa kiwango walichoonesha wachezaji wake wakati wa
mazoezi ana imani watakwenda kuwashangaza wengi.
“Timu ipo kwenye hali nzuri mno, nadhani hata Afrika Kusini watatuogopa, tunataka kurejea na kombe,” alisema.
Nahodha Victor Joseph alisema wamejiandaa vema na kwamba wanakwenda
kuwania kombe na hawana shaka watalileta Tanzania. “Mtazamo wetu ni
kurejea na kombe, tupo vizuri, mazoezi tuliyopata yametusaidia mno,”
alisema.
chanzo: habari leo
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment