netball

TANZANIA YA POROMOKA KIMATAIFA

WAKATI Uganda na Zambia zimepanda katika viwango vya netiboli kimataifa, Tanzania ambayo imeshindwa kushiriki mashindano kadhaa kutokana na ukata, imeporomoka hadi nafasi ya 15 sasa.

Kwa mujibu wa viwango vilivyotolewa na INF wiki hii, Tanzania sasa iko nafasi ya 15 wakati kwa muda mrefu ilikuwa katika nafasi ya 14, lakini iliwahi kufikia hadi ya 12 na Uganda ilikuwa chini ya Tanzania kwa ubora.

Taarifa hiyo ya NIF imesema kuwa Uganda imepanda hadi katika nafasi ya 13 na hii inatokana na nchi hiyo kushiriki mashindano mengi na kufanya vizuri ikiwemo kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwakani nchini Australia.

Tanzania katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu sasa imeshindwa kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa yakiwemo ya Mataifa nchini Singapore, Afrika yaliyofanyika nchini Malawi ya vijana yaliyofanyika Botswana na yake ya kufuzu kusaka tiketi ya Kombe la Dunia yaliyofanyika Gaborone kuanzia Septemba 14 hadi 20.

Taarifa hiyo ya INF imesema kuwa viwango hivyo vimetokana na mechi za kimataifa zilizochezwa hadi Septemba 19, mwaka huu, na kufuatia kumalizika kwa mashindano ya Afrika ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Kutokana na kiwango walichoonesha katika mashindano hayo ya kufuzu, Uganda imepanda nafasi mbili kutoka ya 15 iliyokuwa awali hadi nafasi ya 13, huku Zambia ikipanda nafasi nne kutoka 22 hadi ya 18.

Australia ndio inaongoza katika viwango hivyo vya ubora ikifuatiwa na New Zealand huku England ikishuka nafasi ya tatu na Jamaica ni ya nne wakati Malawi iko katika nafasi ya tano na Afrika Kusini ni ya sita.

Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Annie Kibira alisema wanaangalia uwezekano wa kucheza mechi kadhaa za kimataifa na timu zilizoko katika nafasi ya juu katika viwango ili kuiwezesha Tanzania nayo kupanda.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.