basketball

CBE, UDSM KUCHUANA KATIKA BBALL KITAA

TIMU za mpira wa kikapu zenye upinzani mkali Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), zitapambana kesho katika sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa mashindano ya Bball Kitaa.

Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Upanga jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo yamekuwa yakidhaminiwa na kinywaji cha Sprite.

Mratibu wa mpambano huo, Karabani Karabani alisema timu zote zipo katika mazoezi makali kujiandaa na mechi hiyo ambayo inatarajiwa kuwa ngumu na ya kusisimua.

“Hii ni mara ya pili CBE na UDSM wanakutana mwaka huu, baada ya CBE kuibuka washindi katika mechi iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Januari,” alisema Karabani.

“Tunajivunia mafanikio ya mashindano haya ya BBall Kitaa ambayo yametoa mchango mkubwa katika kuhamasisha na kukuza vipaji vya wachezaji, wengi wao wakiwa ni wanafunzi kutoka vyuo vikuu,” aliongeza Karabani.
Kwa upande wake, Meneja Bidhaa Msaidizi wa Coca-Cola Tanzania, Warda Kimaro alisema kampuni hiyo inajisikia fahari kwa kupewa fursa ya kusaidia maendeleo ya mpira wa kikapu nchini Tanzania na alielezea dhamira ya kampuni ya Coca-Cola kuendelea kushirikiana na wadau wa mpira wa kikapu katika kukuza mchezo huo.

“Tunaelewa kwamba mpira wa kikapu ni moja ya michezo maarufu sana hapa Tanzania hasa miongoni mwa vijana, ambao wanahitaji aina ya msaada huu, ili waweze kuendeleza vipaji vyao,” alisema Kimaro.

Sprite imekuwa ikidhamini mashindano ya BBall Kitaa tangu mwaka jana katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.

Michezo hiyo ambayo ni maarufu kama Chini Ya Mataa kwa kuwa hufanyika usiku kwa kutumia mwanga wa taa, ilianza Oktoba kwenye Uwanja wa Spider karibu Gymkhana Club.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.