basketball

DODOMA, TEMKE ZAANZA KWA USHINDI KIKAPU TAIFA

MASHINDANO ya Kombe la Taifa kwa mpira wa kikapu yalianza juzi mkoani hapa kwa timu za Dodoma na Temeke kutoa vipigo katika mechi za ufunguzi zilizofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri.

Katika mchezo wa kwanza kwa wanawake Dodoma waliifunga Mbeya kwa mabao 34-32, mchezo uliokuwa wa vuta nikuvute huku Dodoma wakiongozwa na Imelda Hango aliyekuwa mwiba mchungu kwa wapinzani, Mbeya.

Mpaka mapumziko Dodoma walikuwa wakiongoza kwa mabao 21-16 na katika kipindi cha pili, Dodoma walianza kwa kasi na kupata mabao ya haraka haraka kupitia kwa Hango huku Mbeya wakijibu mashambulizi lakini bahati haikuwa upande wao.

Katika mchezo wa jioni, Temeke iliifunga Dodoma kwa upande wa wanaume kwa mabao 40-18 ambapo mchezo huo ulitawaliwa na Temeke ambapo wachezaji wake walionekana kuwazidi ujanja Dodoma na kuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mitupo mitatu.
Awali akifungua mashindano hayo, Diwani wa Kata ya Mnadani, Steven Masangia alisema sasa serikali inatakiwa kuona umuhimu wa kurudisha mchezo wa Kikapu katika shule za msingi ili vijana wengi wapate fursa ya kufahamu mchezo huo tangu wakiwa wadogo.

“Vijana wakiandaliwa vyema tangu wakiwa wadogo wataleta mapinduzi makubwa katika mchezo huu,” alisema.

Alisema michezo kwa sasa ni ajira ni lazima Serikali iangalie kwa umakini ili vijana wengi waweze kujiajiri.

Alisema mchezaji wa Tanzania anayecheza kikapu Marekani, Hashim Thabit amepata kujulikana kimataifa kutokana na michezo na kuiletea sifa kubwa Tanzania.

Mashindano hayo yanashirikisha mikoa minane ambayo ni Arusha, Kigoma, Kagera, Temeke, Morogoro, Ngorongoro yenye timu za wanaume, huku Mbeya na wenyeji Dodoma zikiwakilishwa na timu za wanaume na wanawake. 


CHANZO: HABARI LEO

About Unknown

0 comments:

Powered by Blogger.