tenesi

TANZANIA WAPEWA UENYEJI

CHAMA cha Tenisi Tanzania (TTA) kimepewa nafasi nyingine ya kuandaa mashindano ya vijana wa ukanda wa Afrika Mashariki kuanzia Januari 11-19, mwakani. Mapema mwaka huu, TTA iliandaa mashindano ya aina hiyo na kufanikiwa kufanya vizuri.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Makamu wa Rais wa TTA Fina Mango, nchi shiriki kwa mwaka 2015 ni Burundi, visiwa vya Comoro, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Shelisheli, Sudan na wenyeji Tanzania.

"Tunategemea jumla ya washiriki wapatao 72 (pamoja na Tanzania). Tanzania itawakilishwa na vijana 22 ikiwa na team A na B… pia TTA inajivunia kuanzishwa kwa mfumo wa renki unaotoa fursa kwa wachezaji kujikusanyia pointi kwenye orodha ya wachezaji wa tennis Tanzania," alisema.

"Hili limesaidia urahisi wa uchaguzi wa timu na kuepuka lawama za kupendelewa watu flani. Kila mchezaji wa chini ya umri wa miaka 18 ana nafasi sawa ya kukusanya pointi kwa kushiriki mashindano yanayoandaliwa na TTA au watu binafsi yaliyoidhinishwa na chama,"alisema.

Alitaja timu ya Tanzania kwa upande wa wavulana itakayoshiriki kwenye michuano hiyo katika umri kuanzia miaka 12 hadi 18 itawakilishwa na Deogratus Ernest, Yusuph Godwin, Kanuti Alagwa, Hassan Yambi, Emmanuel Temba, Ali Hamza, Adam Mwambungu, Frank Mshana, Emmanuel Mallya, Omar Sulle na Hassan Mkajira. Kwa upande wa wasichana ni Easter Nankulange, Emiliana Katabalo, Maria Milanzi, Emiliana Stansilaus, Shadya Kitenge, Jakline Kayunga, Adela Mollel, Georgina Kemmy.

Mango alisema TTA inafanya juhudi kuwataarifu wazazi wa watoto walioingia kwenye timu kwa ajili ya maandalizi.

Timu ya Tanzania itasimamiwa na kocha Nico Jonas ambaye ni msimamizi wa High Performance Tennis (HPC) akishirikiana na Majuto Omari wote wakiwa ni makocha wa level 2 kwa mujibu wa ITF.

Timu inatarajiwa kuingia kambini keshokutwa ambapo watapewa mafunzo mbali mbali pamoja na kufanya shindano la kujipima kabla ya mashindano yenyewe Januari.

About Unknown

0 comments:

Powered by Blogger.