TANZANIA imezidi kung’ara katika mchezo wa tenisi baada ya jana wachezaji wake wawili kutinga fainali katika michuano ya Afrika Mashariki inayoendelea kwenye uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam.
Wachezaji hao ni Deogratias Ernest na Georgina Kemmy ambao walifanya vizuri kwenye mchezo wa nusu fainali na kuwashinda wapinzani wao.
Ernest aling’ara na kutinga fainali baada ya kumshinda mpinzani wake Mtanzania Kanuti Omar kwa seti mbili na kupoteza mchezo mmoja.
Katika robo ya kwanza, Ernest alifungwa na Kanuti seti 7-6, wakati Ernest alishinda michezo miwili kwa seti 6-1, 6-1 na kufanikiwa kuingia fainali ya vijana chini ya umri wa miaka 16.
Aidha, Kemmy alitinga fainali baada ya kumfunga Mrwanda Yabela Omurunga kwa seti 6-1, 6-2. Wachezaji wengine waliofanya vizuri na kuingia hatua ya nusu fainali ni Emmanuel Mallya aliyeshinda michezo miwili na kupoteza mmoja dhidi ya Tabres Kisime.
Alipoteza mchezo wa kwanza seti 6-2, akashinda seti 6-3, 6-2 na kusonga mbele.
Wachezaji wengine ambao mwaka jana waling’ara na kushindwa kufanya vizuri mwaka huu katika mchezo wa robo fainali ni Frank Menard aliyefungwa seti 7-5, 7-5 dhidi ya mpinzani wake Rajab Mtamba. Pia, Omar Sulle alishindwa kung’ara baada ya kufungwa na Muethiopia Yadsir Kibade kwa seti 6-4, 6-3.
Kwa mujibu wa Kocha Majaliwa, Tanzania imefanya vizuri kiasi kwani upinzani umekuwa mkali mwaka huu ukilinganisha na mwaka jana.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment