tenesi

WACHZA TENESI WALIOPO UGHAIBUNI WAREJESHWA

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhs44FUjZvWwBDL1d52_fmeA-7BNvZv-JU8a4WUrp9GR0KKgaoSb_619bSgEdmBEXZwwUFovrDZh_YFhGYujzFIHLBYX-Ny-DTc9uTJVm8kptixn5tnKNM6G5RotMvUhFzV2EYdDjAmz54/s640/DSC_4907.JPG
TANZANIA imelazimika kuwarudisha nchini wachezaji wake wanne chipukizi wa tenisi ambao walikuwa wakihudhuria mafunzo katika vyuo kadhaa vya michezo nchi za nje, ili waje kushiriki kwenye mashindano ya mchezo huo kwa nchi za Afrika, yatakayoanza Jumapili ijayo jijini Dar es Salaam.

Nico Jonas ambaye ameteuliwa kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Tenisi kwa Vijana, na ambaye ni mkufunzi wa mchezo huo kutoka Klabu ya Gymkhana ya Arusha, ameliambia gazeti hili kuwa, wachezaji hao vijana wa kitanzania walikuwa wakijinoa kimichezo katika nchi za Uingereza, Afrika Kusini, Morocco na Burundi na kwamba wanalazimika kurudi kuipiga tafu timu ya taifa kwenye mashindano hayo ya Ukanda wa Mashariki ya Afrika.
Wachezaji hao walioko ughaibuni ni pamoja na Omari Sulle ambaye yuko Casablanca nchini Morocco, Emmanuel Mallya ambaye anajifua jijini Bujumbura nchini Burundi, Mandi Rajab atakayerejea kutoka London, Uingereza na Georgina Kaindoah ambaye anarejea kutoka Johannesburg, Afrika Kusini.

Chama cha Tenisi Tanzania (TTA) kimepewa nafasi nyingine tena ya kuandaa mashindano ya vijana wa ukanda wa Afrika Mashariki (East Africa zonal championships) na yatafanyika kuanzia Januari 12 hadi 18 mwaka huu.

Nchi zitakazoshiriki kwa mwaka huu ni pamoja na Burundi, Comoro, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Seychelles, Sudan na wenyeji Tanzania na inategemewa pia jumla ya wachezaji 72 watashiriki kwenye mashindano hayo huku Tanzania ikiwakilishwa na vijana 22 ikiwa na team A na B.

Wakati huo huo, Chama cha Tenisi Tanzania (TTA) imetangaza kujivunia kuanzishwa kwa mfumo wa renki unaotoa fursa kwa wachezaji kujikusanyia pointi kwenye orodha ya wachezaji wa tenisi Tanzania.

“Hili limesaidia urahisi wa uchaguzi wa timu na kuepuka lawama za kupendelewa watu fulani. Kila mchezaji wa chini ya umri 18 ana nafasi sawa ya kukusanya pointi kwa kushiriki mashindano yanayoandaliwa na TTA au watu binafsi yaliyoidhinishwa na chama,” imebainisha ripoti hiyo kutoka TTA.

Timu ya Tanzania itakuwa na wachezaji 22 na kati ya hao vijana 11 watatoka mkoani Arusha wakiwa ni Nane wa Klabu ya Gymkhana na watatu wa klabu ya AICC. Wengine ni wachezaji kutoka Klabu ya Gymkhana ya Dar es Salaam pamoja na ile ya Kijitonyama.

Timu ya Taifa itasimamiwa na kocha Nico Jonas ambaye ni msimamizi wa High Performance Tennis (HPC) akishirikiana na Majuto Omari, wote wakiwa ni makocha wa daraja la pili kwa mujibu wa Umoja wa asasi za michezo ya tenisi duniani (ITF). 


CHANZO: HABARI LEO

About Unknown

0 comments:

Powered by Blogger.