Bendera hiyo imekabidhiwa na Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Uaskari Moshi, MPA, Matanga Mbushi, ambapo michuano hiyo itashirikisha nchi sita, kwa lengo la kutafuta nafasi ya kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola.
Mbushi, ambaye chuo chake kitatumika katika michezo hiyo, aliwataka wachezaji hao kutambua kuwa kukabidhiwa bendera ya Taifa ni sawa na kukabidhiwa umma wa Watanzania, hivyo ni vyema wakajituma kwa kutambua macho ya nchi yapo nyuma yao.
Alisema licha ya mchezo huo kutopewa kipaumbele kama soka, jitihada zinahitajika kukuza na kuhamasisha mchezo huo, ikiwa ni pamoja na kuandaa maeneo maalumu ambayo mchezo huo unaweza kufanyika na wananchi wakaudhuria.
Mbushi alisema mbali na kupewa jukumu la kukabidhi bendera ya Taifa kwa timu hiyo, lakini changamoto ya michezo ni kubwa kwani hakuna kiongozi yeyote kutoka ngazi wizara, mkoani na wilayani ambao walifika katika kutoa ushirikiano, ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa na ari ya kufa vizuri.
“Hii ni timu ya taifa na inawakilisha nchi yetu kwenye haya mashindano makubwa, mwaka jana walikabidhiwa bendera na Rais Jakaya Kikwete, kutokana na hamasa ile waliweza kuwa mabingwa, kwa mwaka huu tumekubali kupokea mashandano hayo kama wenyeji, lakini tunakabidhi timu bendera hakuna hata kiongozi mmoja wa michezo aidha kutoka wizarani, mkoani hata wilayani,” alisema Mbushi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Judo Tanzania (JATA), Innocent Mallya alisema kikosi chake chenye wachezaji 23, kimejiandaa vizuri katika kutetea ubingwa wao walioutwaa Kenya mwaka jana.
Mallya alisema nchi zitakazoshiriki katika mashindano hayo, ni wenyeji Tanzania, Zanzibar, Kenya, Burundi, Rwanda na Ethiopia, huku akitamba ubingwa kubaki nyumbani kutokana na morali ya wachezaji na nidhamu ya hali ya juu.
Pia alipongeza uongozi wa MPA kujitokeza kudhamini timu hiyo kwa kukubali kuweka kambi ya wiki mbili pamoja na kukubali mashindano hayo yafanyike chuoni hapo.
0 comments:
Post a Comment