gofu

SHEIN AFUNGUA UWANJA ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amefungua kiwanja kipya na cha kisasa cha mchezo wa gofu na kusema kuwa ufunguzi huo unakwenda sambamba na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Awamu ya Saba ya kufufua michezo nchini.

Dk Shein aliyasema hayo, katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Utawala Bora, Dk Mwinyihaji Makame katika sherehe za ufunguzi wa kiwanja cha mchezo wa gofu katika Hoteli ya Sea Cliff, iliyopo Kiombamvua, wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja juzi.

Alisema lengo na jitihada hizo ni kuona kuwa vuguvugu la michezo linarejea Zanzibar na kutoa wanamichezo wenye vipaji mbalimbali wenye uwezo wa kushinda katika mashindano ya kimataifa.

Alisema imani yake ni kuwa uwanja huo wa gofu utaiwezesha Zanzibar kuwa na wanamichezo wenye vipaji vya kucheza mchezo huo na kushinda katika michuano ya kimataifa.

"Bado ni mapema kufikia kuwa na Tiger Woods kutoka Zanzibar, lakini hakuna sababu ya kuondoa matumaini kwamba hatuwezi kuwa na mchezaji mahiri katika mchezo huo," alisema Dk Shein.

Aidha, Dk Shein alisema ufunguzi wa kiwanja hicho cha gofu utachangia katika kurejesha sifa na umaarufu wa Zanzibar katika michezo ukiwemo wa gofu.

"Nafahamu kwamba hivi sasa si watu wengi wanaofahamu kuwa Zanzibar ilikuwa ni miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa barani Afrika kuwa na kiwanja cha mchezo wa gofu ambacho kilikuwa katika eneo la Mnazi Mmoja, Mivinjeni hadi upande wa uwanja wa Maisara, Mjini Unguja," alisema Dk Shein.

Pamoja na hayo, Dk Shein alisema amefurahi kupata taarifa kuwa wamiliki wa hoteli hiyo hawaoni kama kiwanja hicho ni mali yao pekee yao, bali wanaona kama ni mali ya Zanzibar na watu wake wote kutokana na kupata hisia kuwa kuzingatia kuwa uzuri wa kiwanja hicho, utatumika kuitangaza Zanzibar kiutalii na kimichezo duniani kote.

Alisisitiza kuwa ni dhahiri kuwa ufunguzi wa kiwanja hicho unakwenda sambamba na juhudi zinazochukuliwa na SMZ Awamu ya Saba za kuimarisha sekta ya utalii ambayo ndio sekta kiongozi kwa uchumi wa Zanzibar.

About Unknown

0 comments:

Powered by Blogger.