mingine

TANZANIA HOI WAVU UFUKWENI

http://ichef.bbci.co.uk/news/ws/304/amz/worldservice/live/assets/images/2015/01/26/150126043631_mpira_wavu_304x171_bbc_nocredit.jpg
TANZANIA imeendelea kufanya vibaya katika mashindano ya kimataifa baada ya timu zake kushindwa kutamba katika mashindano ya mpira wa wavu wa ufukweni ya Kanda ya Tano ya Afrika yaliyomalizika jana jijini Dar es Salaam.

Na badala yake Kenya na Burundi ndizo zilizofuzu kucheza hatua ya pili ya Kanda ya Afrika mashindano yatakayofanyika baadae mwaka huu ili kupata timu za Afrika zitakazoshiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Rio de Janeiro, Brazil mwakani.

Mashindano hayo yaliyoanza juzi katika ufukwe wa Mbalamwezi Club Mikocheni jijini Dar es Salaam, yalishirikisha nchi za Tanzania, Kenya na Burundi huku Ethiopia, Djibouti na Somalia zikishindwa kushiriki.

Tanzania pamoja na kuwa mwenyeji imeshindwa kupata timu itakayocheza hatua ya pili ya mashindano hayo yatakayoshirikisha Kanda Saba za Afrika ili kupata timu mbili zitakazofuzu kwa Olimpiki nchini Brazil mwakani.

Baada ya kuanza vizuri siku ya ufunguzi kwa wanawake, jana timu zote za Tanzania ziligeuka nyanya na kujikuta zikipoteza michezo yao yote na kushindwa kupata pointi za kutosha ambazo zingewavusha katika raundi hiyo.

Katika mchezo wa kwanza jana timu ya Tanzania One ya wanaume ilijikuta ikipoteza mchezo wake baada ya kufungwa 2-0 na Kenya Two huku washindi wakishinda 21-13 na 21-17 katika seti ya kwanza na pili.

Katika mchezo mwingine Tanzania One ya wanawake ilipokea kichapo cha 2-0 kutoka kwa Kenya Two huku washindi wakitoka kifua mbele kwa 21-19 na 21-19 katika seti ya kwanza na pili.

Wanaume wa Tanzania Two walipokea kichapo cha 2-0 kutoka kwa Kenya huku washindi wakishinda kwa 21-10 na 21-18 na timu ya wanawake ya Tanzania Two ilipokea kipigo kingine cha 2-0 kutoka kwa Kenya One.

Washindi walishinda 21-12 na 21-13 wakati Kenya One wanaume waliigalagaza Tanzania One kwa 2-0 huku washindi wakitamba kwa 21-8 na 21-18. Timu za Tanzania zilidhaminiwa na Kampuni ya vinywaji ya Black Energy.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.