BONDIA wa Tanzania Francis Cheka atamba kuwa anao uwezo wa kumshinda mpinzani wake Mthailand Kiatchai Singwancha katika pambano la raundi 10 litakalopigwa leo kwenye uwanja wa PTA Sabasaba.
Akizungumza jana wakati anapima uzito, Cheka alisema kitendo cha kupelekwa jela hakijamuathiri kiasi cha kukubali kushindwa kiurahisi, kwani amefanya maandalizi ya kutosha yatakayompa ushindi.
Alisema: “Ni kweli nimetoka jela lakini haimaanishi kuwa nimepoteza ubora wangu, nimejipanga muda mrefu naamini kuwa nitatoa kipigo kwa mpinzani wangu.”
Naye Mthailand Kiatchai alisema yuko vizuri kwani hana mengi ya kuzungumza zaidi ya kusubiri vitendo leo. Promota wa pambano hilo, Kaike Siraju alisema mambo yote yamekamilika na kuhimiza mashabiki wa mchezo kujitokeza kwa wingi kushuhudia kwa vitendo na kumshangilia Cheka.
“Tunamuombea Cheka ashinde lakini inahitajika nguvu ya mashabiki watakaomshangilia kwa wingi leo,”alisema.
Bondia huyo Mthailand amecheza jumla ya michezo 47 ameshinda 35 na kati ya hayo, ameshinda 16 kwa ‘Knockout’ (KO) akipoteza 12 na kupigwa tisa KO.
Wakati Cheka ameshacheza michezo 40 na kati ya hayo ameshinda 30 na kati ya hayo 16 kwa KO, akipoteza nane na sare mbili.
Aidha, bondia Kassim Ouma wa Uganda alishindwa kutokea kupima uzito bila promota Kaike kujua sababu, akisema tayari alishatuma tiketi ila kinachomshangaza ni ukimya na Mkenya Fred Nyakas naye pia ameshindwa kufika kutokana na kuwa na mgogoro na promota wake.
Kutakuwa na mapambano mengine ya utangulizi kati ya Twaha Kiduku dhidi ya Seleman Zugo, Cosmas Cheka dhidi ya Fred Nyakas, KCY Amar dhidi ya Vicent Mbilinyi, Ibrahim Maokola dhidi ya Joseph Sinkala na baadhi ya wengine.
0 comments:
Post a Comment