ngumi

KLABU BINGWA NGUMI YASOGEZWA MBELE

MASHINDANO ya klabu bingwa ya taifa ya ngumi yaliyopangwa kufanyika mkoani Kigoma kuanzia Mei 17 hadi 24, huenda yakaahirishwa baada ya uongozi wa mkoa kuomba muda zaidi wa maandalizi, imeelezwa.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita zilisema kuwa, Chama cha Ndondi Mkoa wa Kigoma, ambao ndio wenyeji wa mashindano hayo wameomba yasogezwe mbele ili wapate muda zaidi wa maandalizi.

Taarifa hiyo ilisema kuwa mkoa wa Kigoma umeliomba Shirikisho la Ndondi Tanzania (BTF) kusogeza mbele mashindano hayo hadi Juni 10-16 ili wajipange vizuri kuandaa mashindano hayo.
Imeelezwa kuwa uongozi wa BFT bado haujakubaliana na ombi hilo la Kigomala kuyasogeza mbele mashindano hayo, ambayo yatawashirikisha pia mabondia wa timu ya taifa.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa BFT Makore Mashaga alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kuwa maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea vizuri na leo Jumatatu wanatarajia kutoa tamko kamili kuhusu mashindano hayo.

Alisema kuwa kikao cha Kamati ya Utendaji kilichopangwa kufanyika Ijumaa iliyopita jijini Dar es Salaam kilishindwa kufanyika baada ya wajumbe wa BFT kutotimia.

Aidha, Mashaga akizungumzia kuhusu timu ya taifa inayoendelea na mazoezi kwenye uwanja wa taifa wa ndani alisema inaendelea vizuri na wanatarajia kuanzia leo Jumatatu kasi ya mazoezi itaongezeka kwa timu hiyo iliyo chini ya makocha wanne.

Timu hiyo yenye mabodia 17 iko chini ya kocha mkuu Benjamin Mwangata anayesaidiwa na Jonas Mwakipesile, Said Omary `Gogopoa’ na Mussa Mwaisori.

Chanzo: Habari leo

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.