maproo

KIIZA: SIMBA ITANIREJESHA TIMU YA TAIFA



Mshambuliaji mpya wa Simba, Hamisi Kiiza, amesema atafunga kila atakapopata nafasi na kwamba hiyo ndiyo kazi iliyomleta katika klabu hiyo yenye makao makuu yake mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Kiiza ambaye ametua Simba akitokea Yanga, juzi jioni aliifungia Simba bao la kwanza katika ushindi wa 2-1 kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Kombaini ya Zanzibar.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu kutoka Zanzibar, Kiiza alisema anafanya mazoezi kwa bidii ili kurejea katika kiwango chake cha juu na hatimaye Simba kufurahia usajili wake.

Kiiza alisema atakapofanya vizuri, ataisaidia klabu yake hiyo ya Simba na yeye anahitaji kurejea kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda (Cranes).

Bao la pili katika mchezo huo lilifungwa na mkongwe aliyerejea, Mussa Hassan 'Mgosi' ambaye naye alidhihirisha kwamba bado kiwango chake kiko juu na ataisaidia Simba msimu ujao.

Mechi hiyo ni ya kwanza kwa Simba kwa Muingereza na Kocha Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Dylan Kerr ambaye amechukua mikoba ya Mserbia, Goran Kopunovic, aliyeondoka baada ya kushindwa dau la mkataba mpya.

Ushindi huo unaifanya Simba kuanza vizuri kwa maana ya mechi za kirafiki baada ya kutocheza mechi yoyote ilipokuwa Lushoto, mkoani Tanga.

Kikosi hicho kitacheza mechi nyingine mbili kabla ya kurejea jijini tayari kuwakabili Wakenya AFC Leopards katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Agosti 8, mwaka huu (Simba Day) kwenye Uwanja wa Taifa 

CHANZO: NIPASHE

About kj

1 comments:

Anonymous said...

Tunataka taarifa za mnyama tu!

Powered by Blogger.