netball

MWAKA WA SHETANI, TAIFA QUEENS WACHAPWA ZOTE BOTSWANA

TIMU ya taifa ya netiboli ya Tanzania, Taifa Queens, imetoka mikono mitupu katika mashindano ya Afrika nchini Botswana baada ya kufungwa mechi zote nne.

Taifa Queens wakati wa kuanza mashindano hayo Jumapili iliyopita, ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kutokana na kuwa juu kiviwango vya mchezo huo duniani, ukilinganisha na timu zingine shiriki.

Tanzania ni ya 15 kwa viwango vya ubora kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Netiboli (INF), huku ikifuatiwa na wenyeji Botswana ambao wako katika nafasi ya 16, Zambia (18), Zimbabwe (26), Namibia (31) na Swaziland (33).

Kwa mujibu wa toleo la jana la gazeti la Herald la Zimbabwe, timu ya taifa ya Zimbabwe ilitwaa taji hilo la Afrika baada ya kushinda mchezo wa mwisho kwa mabao 37-28 dhidi ya Taifa Queens.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, washindi walikuwa mbele kwa mabao 19-14 huku robo ya tatu, Zimbabwe ilikuwa mbele kwa 30-18 na Taifa Queens ilimaliza robo ya mwisho ikiongoza kwa 8-7.

Katika mashindano hayo ambayo ni ya kwanza kushiriki tangu uongozi mpya wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) ulipoingia madarakani zaidi ya miaka miwili iliyopita, Taifa Queens ilianza kwa kufungwa na Zambia kwa mabao 55-37.

Timu hiyo iliyokwenda Botswana kwa ufadhili wa Covenant Bank iliyotoa kiasi cha Sh milioni 40, ilifungwa tena wenyeji Botswana 47-39 kabla ya kupigwa na wachovu Swaziland kwa mabao 47-44 na kumaliza kwa kufungwa na Zimbabwe.

Taifa Queens ilifungwa na Zambia mabao 55-37 kabla ya kuchapwa tena na wenyeji Botswana kwa 47-39 na kupigwa 47-44 na Swaziland kabla ya kuhitimisha vipigo kwa kugaragazwa kwa mabao 37-28 na Zimbabwe.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.