ngumi

MASHALI ASHINDWA KUTOKEA UPIMAJI WA UZITO

Thomas Mashali
BONDIA Thomas Mashali jana alishindwa kutokea kwenye upimaji uzito kwa ajili ya mpambano wake wa leo dhidi ya Ibrahim Tamba utakaofanyika kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam. Pambano lao litatanguliwa na mapambano ya awali 10.

Katika tukio la jana ambalo mabondia wengine wote walijitokeza kwenye upimaji huo wa uzito akiwamo Tamba, lakini Mashali hakutokea licha ya kuwa waliambiwa wajitokeze saa tatu nusu asubuhi.

Mratibu wa mpambano huo,Kaike Siraji alisema amekuwa akimsihi Mashali tangu juzi kujitokeza kwenye upimaji huo, lakini bondia huyo hadi muda unafika hakupiga simu kutoa udhuru wala alikuwa hajibu ujumbe wa maneno.

Siraji alisema kuwa kwa taratibu ni lazima mabondia wajitokeze kupima uzito pamoja na kwa kushindwa kujitokeza kwa wakati, hatocheza mpambano huo hadi atakapopimwa hata akiwa peke yake.

“Najua kesho (leo) ndio mpambano sasa shangaa kuona kuwa mtu huyu hadi sasa hajafika katika upimaji na najua hiyo sio inavyotakiwa kabisa katika kazi hizi za ubondia,” alisema Siraji akizungumzia pambano hilo lisilo la ubingwa.

Alisema kiingilio kitakuwa Sh 10,000 na 15,000 na mgeni rasmi ni bondia maarufu nchini, Francis Cheka wa Morogoro.

Akizungumzia kuhusu mapambano ya awali, alisema kuwa Cosmas Cheka atapambana na Rashid Matumla, Nassib Ramadhan atakumbana na Boxer Mnyama, Karama Nyilawila atapambana na Shaban Kaoneka wakati mabondia wanawake, Halima Bakari na Mwanne Juma wataoneshana kazi.

Mratibu huyo alisema kutakuwa na ulinzi mkali na kuahidi kuwa hakutakuwa na vurugu kama ilivyozoeleka.

“Huu ni mpambano wenye hisia mbalimbali kwa kuwa wapenzi wa ngumi wenyewe kwanza wameshajipanga kushabikia timu zao na kwa hiyo watu wanaweza fikiria kuwa kutakuwa na fujo kitu ambacho nawahakikishia kuwa kutakuwa na ulinzi,” alisema Siraji.

Alisema kila bondia ameshalipwa stahiki zake na kuwa kila bondia yupo tayari kwa mpambano huo.

Chanzo: Habari leo

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.