CECAFA

STARS KUWAKABILI ETHIOPIA CHALENGE


TIMU ya soka Taia ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ itacheza na Ethiopia katika robo fainali ya Kombe la Chalenji kesho.

Kilimanjaro Stars jana ilimaliza hatua ya makundi ya michuano ya Chalenji inayoendelea nchini Ethiopia kwa kutoka sare ya bao 1-1 na wenyeji wao. Kutokana na matokeo hayo, Kilimanajro Stars inayonolewa na Abdallah Kibadeni imemaliza ikiwa na pointi saba, hivyo kuongoza kundi lake, wakati Ethiopia imeshika nafasi ya tatu.

Kulingana na ratiba ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Stars kwa kuongoza Kundi A itacheza na mshindwa bora (Best Loser) wa pili, ambaye kwa mujibu wa msimamo ni Ethiopia.

Ratiba inaonesha robo fainali ya kwanza kesho mchana itakuwa kati ya Uganda na Malawi, kisha alasiri Kilimanjaro Stars itacheza na wenyeji Ethiopia, mchezo unaotarajiwa kuwa wa vuta nikuvute.

Hatua ya robo fainali itaendelea tena Jumanne, ambapo mchana itakuwa kati ya Sudan Kusini dhidi ya Sudan na alasiri Rwanda itaumana na Kenya. Michuano hiyo inashirikisha timu kutoka Afrika Mashariki na Kati.

Malawi inashiriki kama nchi mwalikwa wa michuano hiyo. Stars imeongoza kundi lake ikiwa na pointi saba, ikifuatiwa na Rwanda yenye pointi sita na Ethiopia yenye pointi nne, huku Somalia ikiwa haijapata pointi.

Katika mchezo wa jana, Stars ilipata bao lake dakika ya 51, mfungaji akiwa Simon Msuva kwa kichwa kutokana na krosi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Stars: Aishi Manula, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Salum Mbonde, Kevin Yondan, Himid Mao, Said Ndemla, Jonas Mkude, John Bocco, Elias Maguli na Simon Msuva.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.