CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kinakusudia kufanya ukarabati mkubwa kwenye viwanja vyake mbalimbali vya michezo nchini ili vilingane na hadhi ya chama hicho.
Ahadi hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye wakati akikagua Uwanja wa Namfua utakaotumika katika sherehe za Maadhimisho ya miaka 39 ya CCM yaliyopangwa kufanya Kitaifa mkoani hapa Februari 06 mwaka huu.
Nape alisema CCM inamiliki viwanja vya michezo karibu nchi nzima, lakini ni vichache tu ndio ambavyo vina hadhi ya kutumika kwa ajili ya michezo ya kimataifa. “Bahati nzuri viwanja vyote vya CCM viko chini ya Idara ya Itikadi na Uenezi ambapo mimi ndio mkuu wake wa Idara.
Tumekusudia kuvifanyia ukarabati mkubwa viwanja vyetu vyote ili viweze kutumika kwa michezo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa,” alisema Nape. Hata hivyo, alisema kuwa ukarabati huo utafanyika kwa awamu kutokana na idadi kubwa ya viwanja hivyo.
Viwanja hivyo ambavyo hutumika kuchezewa mechi mbalimbali zikiwemo za Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na hata Ligi za Mabingwa wa mikoa ni Mkwakwani Tanga, Sheikh Amri Abeid, Arusha na Jamhuri Morogoro.
Vingine ni CCM Kirumba Mwanza, Kambarage Shinyanga, Sokoine Mbeya, Kaitaba Bukoba, Namfua Singida, Ali Hassan Mwinyi Tabora, Jamhuri Dodoma, Samora Iringa, Majimaji Songea na Lake Tanganyika Kigoma.
Akizungumzia Uwanja wa Namfua, Waziri huyo alisema kuwa mipango ya kuurabati uwanja huo imekamilika, ikiwemo shughuli ya kusaini mikataba ya ujenzi baina ya CCM na wadau wake mbalimbali.
“Ujenzi wa uwanja huu ilikuwa ni ahadi ya Uchaguzi ya mwaka 2010. Safari hii tumeamua kuujenga kisasa zaidi, ikiwa ni pamoja na kuuwekea nyasi bandia na uzio kuzunguka uwanja wote,” alisema Nape na kusisitiza kuwa ujenzi utaanza mara baada ya maadhimisho kumalizika.
Hata hivyo, Waziri huyo alikataa kutaja gharama wala muda wa kukamilisha ujenzi wa uwanja huo huku akidai kuwa gharama ni makubaliano baina ya chama na wadau.
Chanzo: Habari leo
0 comments:
Post a Comment