Jumla ya Sh. milioni 224 zimepatikana kutokana na mechi 15 zilizochezwa katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu huko Kisiwani Unguja, Zanzibar imeelezwa.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa Kamati ya Mashindano hayo, Khamis Said Abdallah, alisema kuwa kati ya fedha hizo, jumla ya Sh. milioni 223 zimetumika kulipia gharama za kuendesha michuano hiyo.
Abdallah alisema kuwa timu zote nane zilizokuwa zinashiriki mashindano hayo zililipiwa gharama za usafiri, malazi na chakula kwa muda wote waliokuwa wakishiriki michuano hiyo iliyoanza kufanyika mwaka 2007.
Katibu huyo alisema kuwa michuano ya mwaka huu ilikuwa na changamoto mbalimbali na moja yapo ni kukosa fedha za kutoa zawadi ya mfungaji bora, refa bora na tuzo nyingine zinazoendana na hadhi ya michuano.
"Jumla ya fedha zilizokusanywa na kamati ni Sh. milioni 224 na tumetupia Sh. milioni 223, ndiyo maana hata zawadi ndogo ndogo mwaka huu tumeshindwa kuzitoa kwa wachezaji na wadau wetu walioshiriki," alisema Abdallah.
Alieleza kuwa kukosekana kwa mapato mengi uwanjani mwaka huu kulisababishwa na kutopatikana kwa wadhamini wengine na hali ya kisiasa iliyopo visiwani humo.
Timu ya URA kutoka Uganda ndiyo imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mwaka huu kwa kuifunga Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro mabao 3-1 katika mchezo wa fainali.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment