kitaa

KWA HILI MKWASA UMECHEMKA, HONGERA 'CANAVARO'!


Nadir Haroub 'Canavaro', ametangaza rasmi kustaafu kucheza soka la Kimataifa, ni uamuzi wa kushtukiza lakini naamini 'Canavaro' amefanya maamuzi sahihi.

Ametaja sababu kadhaa zilizopelekea maamuzi hayo, moja ya sababu hizo ni kuvuliwa unahodha 'kihuni' ndiyo ni kihuni, maana wahusika wameshindwa kuthamini mchango wake, tukumbuke Nadir Haroub 'Canavaro' ameitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa miaka kumi mfululizo, akiwa na nidhamu ya hali juu, akijituma mithili ya mtu aliyejitoa 'jihad' (kufa na kupona) halafu mwisho wa siku wahusika wanatengua unahodha wake kwa kutumia vyombo vya habari eti kisa nini Samatta!

Nadhani tuna tatizo la kufikiria, ni kweli Mbwana Ali Samatta ameipa heshima kubwa Tanzania baada ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani lakini ukweli usiopingika mchango wa 'Canavaro' katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ni mkubwa kuliko Samatta, wahusika wamekurupuka kwa kumpa Samatta unahodha wa Timu ya Taifa huku wakimvua 'kihuni' Canavaro.

Ilitosha kuthamini mchango wake kwa kumwandalia hafla maalum ya pongezi kwa uongozi wake uliotukuka ndani ya kikosi cha Taifa Stars, matokeo yake 'wahuni' hawa (kumradhi) wakamchinjia baharini, kisa Mbwana Samatta, kweli? Mbona tuna baadhi ya viongozi wajinga kiasi hichi? Watu wameshindwa kutofautisha tuzo ya Samatta na uongozi wa Nadir Haroub ndani ya Stars! Hivi kabla ya maamuzi huwa tunafikiri kwa kutumia akili au makalio?

'Canavaro' ambaye ameichezea Timu ya Taifa ya Tanzania kwa takribani miaka 10, ameamua kutangaza kustaafu kuichezea Timu ya Taifa, Canavaro ametaja sababu kadhaa zilizomfanya afikie maamuzi hayo, ikiwemo sababu ya kuvuliwa unahodha bila ya heshima yoyote, licha ya kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu (miaka kumi).

Inawezekana ni maamuzi ya hasira lakini lawama tuzipeleke kwa waliochochea hizo hasira, vyovyote itakavyokua tuzo ya Samatta na ukubwa wake na thamani yake na heshima yake lakini haiwezi kulipa kujitolea kwa Nadir Haroub ndani ya Taifa Stars hata siku moja, haikustahiki hata kwa bahati mbaya kuuvua unahodha wa 'Canavaro' kihuni kupitia 'media' ukamchagua Mbwana Samatta kisa tuzo!

Yalitakiwa yaandaliwe mazingira rafiki kwa Nadir Haroub kuthamini mchango wake kwa Taifa sio kumfanyia uhuni wa kiwango cha 'masters', hili linaweza kuchangia kuporomoka kiwango cha Timu ya Taifa, maana ikumbukwe 'Canavaro' alikuwa kiongozi kwa wenzake na kitendo alichofanyiwa si cha kiungwana hivyo kinaweza kuwaambukiza na wachezaji wengine.

Ifikie wakati tuwe na viongozi wenye uwezo mzuri wa kufikiri na kufanya maamuzi yenye tija na yanayoelekea kuleta mabadiliko chanya badala ya viongozi wanaoongozwa na utashi wa kilofa.

Naomba kuwasilisha!
Ahsante!
Ally Mohammed,
Zanzibar,
Tanzania.
Barua-pepe, allymohammed01@gmail.com

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.