mtazamo

MKWASA AMSHANGAA NADIR HAROUB


KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars Charles Mkwasa amesema kuwa anashangaa kusikia kuwa, Nadir Haroub Cannavaro ameamua kujitoa timu ya taifa kwa sababu ya kuvuliwa unahodha wa timu hiyo.

Hivi karibuni Mkwasa alimpa unahodha mchezaji wa TP Mazembe ya Congo DR, Mbwana Samatta na kusema Haroub atabaki kuwa nahodha kwenye timu inayoshiriki michuano ya ndani ya Afrika (Chan).

Uamuzi huo ulimfanya Haroub kutangaza kujiuzulu kucheza timu ya taifa, akisema moja ya sababu ni kupokwa nafasi hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkwasa alisema anamheshimu Haroub na anatambua mchango wake kwenye taifa.

“Sikuwa na sababu ya kumwondoa kwenye unahodha, mimi namheshimu sana Canavaro (Haroub) na ametoa mchango mkubwa kwa taifa hili na bado namhitaji, kwa nini nimuondoe,” alisema.

“Nilichokifanya ni mabadiliko kidogo tu kwenye kazi, ni kama ninyi huko kuna mhariri wa habari na mhariri wa michezo, ndivyo nilivyofanya mimi na hili lipo duniani kote, hata ukiangalia wenzetu Ivory Coast, Cameroon, Zambia, Uganda na hata Rwanda… “Sasa hivi kuna mashindano ya Chan yanaendelea lazima utakuta na hodha wa Afcon sio yule wa Chan,” alisema.

Akifafanua zaidi Mkwasa alisema aliamua kumpa Samatta ili kuwa, kama motisha zaidi baada ya kupata tuzo ya mwanasoka bora anayecheza Afrika.

“Na ili hata akienda huko nje thamani iongezeke kwamba hachezi tu timu ya taifa lakini pia ni nahodha,” alisema.

“Halafu si kweli kwamba Canavaro alipata taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, nakumbuka nilimpigia simu tarehe 10 hata kwenye simu yangu bado inaonesha nikamueleza kwamba nimefanya mabadiliko kidogo yeye atakuwa nahodha wa Chan na Samatta atakuwa wa Afcon, aliniitikia vizuri, lakini kumbe hakufurahi mi sikujua… na sikuona umuhimu wa kumpa barua kwa sababu ni mabadiliko yaliyofanyika ndani ya timu tu humo humo,” alisema.

Kuhusu kujiuzulu kwa Haroub, Mkwasa alisema huo ni utashi wa mchezaji mwenyewe hawezi kumuamulia.

“Si kwamba simhitaji, namhitaji sana kwenye timu yangu, lakini kama ameamua kujiuzulu huo ni utashi wake mwenyewe tu, mimi siwezi kumuamulia, kama ameona uamuzi wake ni sahihi napaswa kuuheshimu pia,” alisema.

Haroub amekuwa nahodha wa Stars kwa takriban miaka 10 akibeba mikoba kutoka kwa Mecky Maxime na Salum Swedi.

Katika taarifa yake mchezaji huyo wa Yanga alisema ameamua kujiuzulu baada ya maneno kuwa mengi hasa kutokana na kipigo cha mabao 7-0 ilichokipata Stars kutoka kwa Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

“Baada ya mechi ile maneno yalikuwa mengi kwamba nimezeeka, umri umekuwa mkubwa hivyo nimeona bora nipumzike, lakini pia suala la kuvuliwa unahodha bila kupewa barua pia sikulifurahia kwani nimecheza kwa miaka 10 kwenye timu hii kwa nguvu zangu zote,” alisema Haroub.

Chanzo: Habari Leo

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.