SERIKALI imesema inafanya mapitio ya sheria iliyounda Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ili iendane na wakati kwa lengo la kuendeleza michezo nchini.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni mjini hapa jana na Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Anastazia Wambura alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde, Khatibu Saidi Haji (CUF), aliyehoji kuhusu sheria za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) zinazokataza masuala ya soka kupelekwa mahakamani.
Mbunge huyo alihoji: “Je serikali inatoa tamko gani juu ya makosa yanayofanyika katika klabu za soka? Je, ni kwa kiasi gani sheria hizo za Fifa zinakinzana na sheria za nchi yetu?”
Akijibu Naibu Waziri, Anastazia Wambura alitaka klabu na mashirikisho ya mpira wa miguu nchini kuzingatia taratibu zilizowekwa na katiba zao kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza katika uendeshaji na uendelezaji wa soka nchini.
“Ni kweli kuwa sheria za Fifa zinakataza mambo yanayohusiana na soka kupelekwa mahakamani,” alisema Wambura.
Alifafanua kwamba, hatua hiyo inalenga kuwezesha masuala yote yanayohusu soka kuendeshwa kwa kufuata na kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa na mamlaka katika ngazi mbalimbali.
Alisema maendeleo ya michezo nchini yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ya mwaka 1967 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 6 ya mwaka 1971.
Hata hivyo, alisema sheria hiyo inatajwa kuwa ni kongwe na ina baadhi ya mambo ambayo yanakinzana na sheria za Fifa na kwamba serikali inafanya mapitio ya sheria hiyo ili iendane na wakati kwa lengo la kuboresha na kuendeleza michezo nchini.
Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo alishutumu baadhi ya viongozi wa michezo kutotii sheria zinazowaweka madarakani na kuiweka Tazania katika hatari ya kufungiwa uanachama wa Fifa na kutolea mfano wa mgogoro wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ambao baadhi ya viongozi wamekimbilia mahakamani na kufanya ZFA itishiwe kusimamishwa uanachama wake na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
“ Fifa wakiamua kuchukua sheria, Tanzania itafungiwa uanachama muda wowote kuanzia sasa. Je, serikali inatoa mwito gani kwa viongozi wasiotii sheria zilizowaweka kwenye mdaraka yao?” Alihoji mbunge huyo kwenye swali la nyongeza.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema viongozi waliopeleka masuala ya michezo mahakamani, taratibu za michezo duniani zinajulikana.
“Kama wapo, kwa kweli hukumu yake kwa Fifa inajulikana. Tutachukua hatua kuhakikisha wanarudi utaratibu wa kawaida kuepusha kufungiwa kwenye michezo,” alisema Nape.
Chanzo: Habari leo
0 comments:
Post a Comment