zanzibar

BMTZ WAFANYA KWELI SULUHU YA ZFA

BARAZA la Michezo la Taifa la Zanzibar (BMTZ) limeunda kamati ya watu sita kuharakisha utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika kikao cha siku mbili.

BMTZ lilikutana Jumatatu na Jumanne wiki hii na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na wajumbe wa Kamati ya Muda ya chama hicho.

Lengo kuu la vikao hivyo ambavyo vilikuwa chini ya Mwenyekiti wa baraza hilo Sharifa Khamis, ni kupitia utekelezaji wa makubaliano yaliyofanyika Novemba 26 mwaka jana.

Walioteuliwa kuunda kamati hiyo ni Rais wa ZFA, Ravia Idarusi, Makamu wa Rais wa ZFA Unguja, Haji Ameir, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Hussein Ali Ahmada, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya ZFA, Masoud Attai, Mjumbe kutoka wilaya ya Magharibi, Mussa Soraga na Mjumbe wa Umoja wa Klabu Haji Issa Kidali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Makamu Mwenyekiti wa BMTZ, Khamis Abdalla Said amesema kuwa kamati hiyo itakuwa na kazi ya kusimamia kwa vitendo utekelezaji wa maazimio yote yaliyofikiwa katika mkutano huo wa siku mbili.

Alisema kikao chake cha kwanza kitafanyika siku ya Jumamosi Uwanja wa Amaan mjini Unguja, ili kuona kuwa mambo yote yanakwenda kwa njia ya maelewano.

Alisema kamati hiyo ya watu sita kwa mujibu wa makubaliano yakifikiwa ndio itakayosimamia maandalizi ya Mkutano Mkuu wa ZFA ambao umepangwa kufanyika si zaidi ya Februari 27 mwaka huu.

Alizitaja ajenda ambazo zitazungumzwa katika mkutano huo ni kujadili mwenendo wa Kamati ya Utendaji ya ZFA, kuteua kampuni ya ukaguzi wa hesabu na kuteua kamati ndogo ya kitaalamu itakayoandika katiba mpya ya ZFA.

Pia kikao hicho kilikubaliana hatua za haraka zichukuliwe katika kufuta kesi moja ya Pemba iliyobakia ya viongozi wa Kamati ya Uchaguzi ya ZFA na pia Rais wa ZFA, Ravia Idarusi kuharakisha kutangaza wajumbe watatu watakaoshirikiana na Kamati inayosimamia ligi.

“Pia katika kikao hicho wajumbe wa pande hizo mbili walikubaliana kufanya kazi kwa pamoja na kuacha kuvutana kwa mustakabali wa kupeleka mbele maendeleo ya soka nchini,” alisema.

Chanzo: Habari leo

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.