zanzibar

JKU KAMILI KUIVAA GABORONE


KLABU ya soka ya JKU ya Zanzibar inatarajiwa kuwasili leo kutoka mafichoni Dar es Salaam ilipoweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa michuano ya kombe la Shirikisho dhidi ya Gaborone United ya Botswana.

JKU ambayo iliondoka Februari 2 mwaka huu, kupiga kambi ya wiki moja itawasili leo kati ya boti ya mchana au jioni na kufikia moja kwa moja kambini kuendelea kujiwinda na mchezo huo uliopangwa kufanyika Jumapili.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Meneja wa timu hiyo Sameja Mohammed Hamad alisema yeye alikuwa pamoja na timu hiyo na amerejea jana kwa ajili ya kuja kuandaa mapokezi ya timu hiyo na mambo mengine.

Alisema kuwa wakiwa katika kambi hiyo walipanga kucheza mechi tatu za kirafiki ambazo walilenga kucheza na Azam FC, Yanga na Simba lakini wote walikataa kwa kila mmoja kutoa sababu zake. Alisema kuwa baada ya kukosa mechi hizo walilazimika kuendelea na programu ya mwalimu ya mazoezi kama kawaida.

“Kwa vile tulikosa mechi na timu hizo tuliweza kuendelea na programu ya mazoezi na vijana wapo sawa na wameiva kwa kushindana,” alisema.

Hivyo alisema kuwa kulingana na wachezaji hao walivyopata mazoezi ya nguvu ana imani kuwa timu hiyo itafanya vizuri na Wazanzibari watarajie ushindi.

Wakati huohuo wapinzani wao Gaborone bado wapo kimya kuhusiana na siku ambayo watawasili visiwani Zanzibar kwa ajili ya mchezo wao wa awali uliopangwa kuchezwa Jumapili ya wiki hii.

Klabu hiyo kwa mara ya mwisho iliwasiliana na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kwa ajili ya kutoa taarifa juu ya kujigharimia kila kitu lakini mpaka sasa hawajatoa taarifa yoyote juu ya lini watawasili.

Hata hivyo habari zilizopatikana jana zilidai kuwa tayari timu hiyo imeshawasili katika ardhi ya Tanzania tangu juzi na kwamba imejificha mahali.

Mwandishi wa habari hizi alipata nafasi ya kuzungumza na Meneja wa timu ya JKU Hamad alisema kuwa mpaka sasa hawajapata taarifa yoyote juu ya wapinzani wao siku ya kuwasili kwao.

Alisema kuwa kwa vile wao wana chama husika ambacho ndicho kinachohusika kuwasiliana nao hawana hofu juu ya hilo na vyovyote vile itakavyokuwa chama chao kitawajulisha.

“Sisi hatupaswi kuwasiliana nao bali ni ZFA ndio wenye jukumu hilo, sisi kila kitu tunasikiliza kutoka kwa viongozi wa chama chetu,” alisema.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.