ngumi

PAZI, MAUGO KUMSINDIKIZA CHEKA


MABONDA Abdallah Pazi na Mada Maugo wanatarajiwa kusindikiza pambano la ubingwa wa mabara kati ya Francis Cheka dhidi ya Muingereza mwenye asili ya Serbia Geard Ajetovic litakalopigwa Februari 27 mwaka huu kwenye viwanja vya Leaders Dar es Salaam.

Pazi na Maugo watapigania mkanda wa mabara katika uzito wa kilo 72 raundi 10 ambapo itakuwa ni mara yao ya kwanza kupigana. Katika pambano hilo litawakutanisha mabondia wengine Ibrahim Class dhidi ya Mohamed Matumla watakaopigana raundi nane.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ulinzi ya Advance ambao ni miongoni mwa wasimamizi wa pambano hilo Juma Ndambile alisema jana Dar es Salaam kuwa mabondia hao Pazi na Maugo tayari wameshasaini mkataba na wako tayari kwa pambano.

“Hii ni nafasi ya pekee kwa mabondia wetu kuonyesha uwezo wao na kuhakikisha wanachukua mkanda wa WBF. Mashali (Thomas) aliwahi kushinda mkanda huo dhidi ya Mada Maugo 2013 akaja kunyang’anywa na Arif Magomedov,” alisema.

Naye Pazi alisema anashukuru Mungu kwa kuonyesha uwezo katika baadhi ya mapambano yake yaliyopita na kwamba ataendeleza ushindi kwa kuhakikisha anamshusha kiwango mkongwe Maugo.

“Namheshimu Maugo kama kaka, lakini siku hiyo hiyo nitamuonyesha kazi kwani ni lazima nimpige kuendelea kujenga heshima yangu,” alisema.

Kwa upande wake Maugo alisema hasira za kushindwa ubunge kwenye uchaguzi mkuu katika jimbo la Rorya mwaka jana atazihamishia kwa Pazi.

“Pazi bado ni kijana mdogo nitamfundisha kazi siku hiyo kwani hasira zangu za kupoteza nafasi ya ubunge zitahamia kwake,” alisema.

Promota wa ngumi za kulipwa Jay Msangi alisema viongozi wa dunia wa WBF na waamuzi kutoka Afrika Kusini wanatarajiwa kutua Februari 23, mwaka huu huku mpinzani wa Cheka Ajetovic akitarajiwa kutua Februari 24 mwaka huu tayari kwa pambano hilo.

Chanzo: Habari leo

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.