SERIKALI imesema itashirikiana na Shirikisho la Ngumi Duniani (WBF) kuweka mfumo bora na kurudisha nidhamu ya mchezo nchini ikiwezekana kuondoa ubabaishaji uliopo kwa lengo la kukuza na kurudisha heshima ya mchezo huo.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye baada ya kufanya mazungumzo mafupi na Rais wa WBF, Howard Goldberg ambaye yuko nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Nnauye alisema wamekubaliana na Rais huyo kukuza mchezo huo katika kutoa mafunzo kwa makocha na mabondia kwa ajili ya kuinua kwa maendeleo.
“Serikali yetu imekusudia kuwekeza katika mchezo huu mbali na soka kuhakikisha tunaweka muundo na mfumo bora, lengo la kwanza ni kurudisha heshima ya mchezo,”alisema.
Nnauye alisema pia wataunda chombo kimoja kitakachosimamia vyama vya mchezo huo nchini na kusaidia kuondoa ubabaishaji na maneno mengi ambayo yapo nyuma ya pazia.
Alisema maneno yaliyoko nyuma ya pazia na ubabaishaji yamekuwa yakichangia kupoteza imani kwa wafadhili hivyo, kazi kubwa iliyopo ni kusafisha mabaya na kutengeneza mfumo utakaowezesha kupata ufadhili.
Katika hatua nyingine, Nnauye alimtakia kila la heri bondia Francis Cheka anayetarajia kupanda jukwaani leo dhidi ya Muingereza Geard Ajetovic pambano la ubingwa wa mabara.
0 comments:
Post a Comment