KILIMANJARO Lager Marathon (Kili Marathon) zimevunja rekodi mwaka huu kwa kuvutia wanariadha zaidi ya 10,000 huku Wakenya wakiendelea kutamba katika mbio hizo.
Katika mbio hizo zilizoanzia Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), na kupita barabara mbalimbali za mji wa Moshi na kushuhudiwa na maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye uwanja huo, Wakenya walitawala kuanzia mbio za Km 42 zinazodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager hadi zile za Km 21 zinazodhaminiwa na Tigo.
Kwenye Km 42 kwa wanaume, mshindi aliibuka Kirui Kiprotich aliyetumia saa 2:16.43 akifuatiwa na Kenneth Ronoh 2:16.48 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Benard Kimaiyo 2:16.52 wote kutoka Kenya.
Kwa upande wa wanawake, bingwa aliibuka Alice Kibor saa 2:38.03 akifuatiwa na Elizabeth Chemweno 2:44.20 huku nafasi ya tatu ikishikwa na Alice Serser 2:44.56 wote kutoka Kenya. Katika Tigo Kili Half Marathon Km 21.1 wanaume, mshindi ni Benard Matheka saa 1:03.23 akifuatiwa na Daniel Muteti 1:03.31 wote kutoka Kenya huku Mtanzania Ismail Juma aliyekuwa mshindi wa mbio hizo mwaka jana akikamata nafasi ya tatu kwa saa 1:03.36.
Kwa wanawake, mshindi aliibuka Grace Kimanzi ambaye pia ndiye aliyekuwa mshindi wa mwaka jana akitumia saa 1:14.08 akifuatiwa na Vicoty Chepkemoi 1:14.51 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mtanzania Failuna Abdi saa 1:14.55.
Kwa upande wa GAPCO Km 10 kwa watu wenye ulemavu baiskeli za magurudumu matatu wanawake, mshindi ni Jorome Safiri 0:59.57 akifuatiwa na Khadija Shabani 1:09.53 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Kuruthum Maulid 1:18.07. Wanaume, mshindi ni Simon Mlelwa saa 0:49.57 akifuatiwa na Benard Matiab 0:50.15 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Vusufu Kibaji.
Kwa upande wa GAPCO Km 10 baiskeli za magurudumu matatu wanaume, mshindi ni Peter Vosta 0:50.48 akifuatiwa na Ebeneza Uron 0:55.48 na nafasi ya tatu ikienda kwa Prosper Cornelly.
Wanawake, mshindi aliibuka Linda Macha 1:25.11 akifuatiwa na Sophia Frank 1:31.50 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Joyce Chuwa 1:38.42. Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akizungumzia mashindano hayo, alisema Serikali inatambua mchango wa wadau wanaoandaa mbio hizo ambazo zimefanyika kwa mara ya 14 mwaka huu.
Alisema kuwa serikali inaendelea kufanya juhudi kuhakikisha wanapata wadau zaidi kwa ajili ya kuboresha mbio hizo katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na zawadi. Nape alisema kuwa Kilimanjaro Marathon, zimekuwa zikipata mafanikio kila mwaka kutokana na idadi ya nchi pamoja wanariadha kuongezeka.
Naye Mkurugenzi wa Masoko wa TBL Group, Kushilla Thomas alisema Kilimanjaro Premium Lager inajivunia kuendelea kuwa mdhamini mkuu wa mbio hizo kwa sababu ya umaarufu wake. Alisema kampuni yake itaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine kufikisha riadha katika kilele cha mafanikio.
Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka alisema kumekuwa na mafanikio makubwa katika mashindano hayo lakini pia yanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Wadhamini wa mbio hizo ni Kilimanjaro Premium Lager, Tigo, GAPCO, Grand Malt, KK Security, Kibo Palace, RwandAir, Kilimanjaro Water, TPC Limited, CMC Automobiles, FNB and Keys Hotel.
Chanzo: Habari leo
0 comments:
Post a Comment