kitaa

ZITTO AANZA MIKAKATI YA KUINUA SOKA LA KIGOMA, AITAKA JKT KANEMBWA AIPANDISHE LIGI KUU


MBUNGE wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT), ametangaza azma ya kuinunua timu ya soka ya JKT Kanembwa inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili, mbunge huyo alisema kuwa tayari ameshaanza mazungumzo na uongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mkoani Kigoma kuona kama upo uwezekano wa kuinunua timu hiyo.

Alisema kuwa mpango wa kuinunua timu hiyo unakuja katika kutekeleza azma ya kuwa na timu ambayo itacheza Ligi Kuu Tanzania Bara na kurudisha hadhi ya michezo ya mkoa Kigoma kwenye soka.

Kabwe alisema kuwa iwapo uwezekano wa kuinunua timu hiyo utafanikiwa mpango utafanywa kuunda kampuni ambayo itakuwa ikisimamia uendeshaji wa timu hiyo kama ilivyo kwa timu ya Azam.

Alisema ni jambo la aibu kuona mkoa wa Kigoma hauna timu hata moja katika Ligi Kuu wakati sehemu kubwa ya wachezaji wanaochezea timu zinazoshiriki ligi hiyo wanatoka Kigoma.

Pamoja na azma hiyo alisema kuwa kama itashindikana kwa timu hiyo kununuliwa kutokana na taratibu za jeshi atatafuta timu nyingine ambayo ataisimamia na kuiwezesha kufanya vizuri ili iweze kucheza Ligi Kuu.

Katika kauli yake Kabwe ametanabaisha kuwa pamoja na mpango wa kuwa na timu ya mpira wa miguu, mpango wake ni kuhakikisha wachezaji wakongwe waliowahi kuchezea timu za madaraja ya juu na timu ya Taifa wakiwemo Juma Kaseja na wengine wanarudi mkoani humo ili kusimamia timu za mkoa huo na kuzifanya ziweze kucheza mashindano ya ligi mbalimbali nchini kwa mafanikio.

Kauli hiyo ya Zitto inakuja siku moja baada ya kuutangazia umma mazungumzo ya awali kati yake na Mkurugenzi wa timu ya Azam FC, Abubakar Bakhresa kuhusu kuanzisha shule ya kuendeleza vipaji Kigoma.

Chanzo: Habari leo

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.