Waogeleaji Josephine”Jojo” Oosterhuis aliyenyosha mkono juu akiwa na wenzake, Isabella Kortland (wa pili waliosimama kutoka kushoto), Jacqulline Kortland ambaye ni pacha wa Isabella (wa tatu kutoka kulia waliosimama) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kunyakua medali tatu katika mashindano ya kuogelea ya Afrika Kusini. Wengine katika picha ni kocha Michael Livingstone (wa kwanza kushoto waliosimama), kocha Alex Mwaipasi (wa pili kulia waliosimama) na meneja wa timu, Inviolata Itatiro wa kwanza kulia waliosimama. Pia katika picha ni Marin de Villard na Celina Itatiro (waliokaa). |
Mbali ya Tanzania na wenyeji, Afrika Kusini, mashindano hayo pia yalishirikisha timu kutoka Zimbabwe, Msumbiji, Angola, na Namibia. Josephine alishinda medali ya dhahabu katika fainali ya mita 100 breaststroke kwa kutumia muda wa 1.21.79 huku Jacqueline alishinda medali ya shaba kwa kushika nafasi ya tatu kwa kutumia muda wa 1.22.91.
Nafasi ya pili ikikwenda kwa Deane Toerien wa Afrika Kusini aliyetumia muda wa 1.22.70 na kutwaa medali ya fedha. Isabella Kortland alishinda medali ya dhahabu kwenye mashindano ya mita 50 katika staili ya backstrokes kwa kutumia muda wa 33.25 kuwashinda Georgy Turner na Zantia Bainabridge wa Afrika Kusini ambao walifungana kwa kutumua muda wa 33.84 kila mmoja.
Waogeleaji Celina Itatiro hakuweza kutwaa medali pamoja na kumaliza akiwa wa tisa kwa kutumia muda wa 1.29.26 katika mita 100 butterfly, Marin de Villard alimaliza wa tisa katika staili ya backstroke kwa kutumia muda wa 37.43.
“Tumefanya vizuri sana, si unajua mashindano haya ni magumu kutokana na ushindani uliopo, Afrika Kusini na nchi nyingine inatumia kutafuta waogeleaji wao ambao watakwenda kushindana katika mashindano ya Cana na wameleta waogeleaji wengi, sisi tumeleta 15 na mpaka sasa tuna medali 3, ni mafanikio,” alisema meneja wa timu hiyo Inviolata Itatiro.Kocha Alex Mwaipasi alisema kuwa wamefurahishwa na matokeo hayo na wanaamini kuwa wakiendelea na msimamo wao wa kushiriki mashindano mengi ya kimataifa, basi watafika mbali sana ndani ya miaka mitano au kumi.
“Mbali ya medali, hapa waogeleaji wanasaka nafasi ya Cana, baadhi ya waogeaji wetu ndiyo kwanza wanaogelea katika bwawa la mita 50, wengine mara ya kwanza, hivyo kuna changamoto,” alisema Mwaipasi.
Kocha Michael Livingstone aliwashukuru wazazi wa waogeleaji kwa kufanikisha safari hii na kuifanya Tanzania kuingia katika chati ya mchezo wa kuogelea. “Wazazi wamejitahidi kwa kweli, wengine wameshindwa na wengine wameambatana na watoto wao kuja hapa kwa ajili ya kuitangaza Tanzania, tumefanikiwa,” alisema Michael.
Chanzo: Michuzi Blog
0 comments:
Post a Comment