kitaa

UTAFITI WA NIPASHE: UZALENDO WA MKWASA WAPITILIZA AJALIPWA MSHAHARA WA MIEZI NANE


'Ndoa' ya kocha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Boniface Mkwasa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huenda ikavunjika wakati iwapo shirikisho hilo halitamlipa kocha huyo mzalendo malimbikizo ya mishahara ya miezi nane kiasi cha Sh. Milioni 200, Nipashe imebaini.

TFF ilisitisha mkataba na kocha wa kigeni kutoka Uholanzi, Mart Nooij Juni 21 mwaka jana baada Stars kunyukwa 3-0 na Uganda Uganda (The Cranes) na kumteua Mkwasa kuchukua nafasi hiyo.

Tangu wakati huo, Mkwasa amelipwa mshahara wa mwezi mmoja tu. Vyanzo vya habari vya ndani zinadai kuwa kocha huyo analipwa mshahara wa Sh. Milioni 25 kwa mwezi.

Hiyo ina maana, tangu Julai mwaka jana hadi leo, kocha huyo mzalendo amelipwa mshahara wa mwezi mmoja tu. Mkwasa aliyeachana na ajira yake Yanga na kutua Stars, sasa analidai shirikisho hilo Sh. milioni 200 kama malimbikizo ya mishahara kwa wakati wote huo.

Chanzo chetu cha habari kilidai kuwa hata mshahara wa Julai, Mkwasa hakulipwa kwa wakati, badala yake alipewa katika awamu tatu.

“Kwa muda wote kocha amekuwa akiishi kwa posho, hajalipwa mshahara kwa muda mrefu. Julai alilipwa katika awamu tatu – Sh milioni 5, 10, kisha wakamaliza kwa kuumpa 10 zingine,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Kilidai kuwa, Juni mwaka jana, Mkwasa alipewa posho wakati timu hiyo ikijiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya The Cranes ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zilizopita za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) ambayo Stars ilitolewa na Waganda hao.

"Ukweli ni kwamba, kocha ana hali ngumu na mambo mengi aliyoahidiwa kwenye mkataba wake hayajatekelezwa hadi sasa,” kiliongeza chanzo chetu cha habari.

Mkwasa alisaini mkataba wa miezi 18 kuinoa Stars ambayo sasa inashiriki michuano ya awali kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani.

“Kwenye mkataba wake, mambo mengi hawajamtekelezea. Kocha amekuwa wakijituma na kufanya kazi kwenye mazingira magumu, lakini hadi leo TFF haijafanya jambo la maana kutekeleza makubaliano.

"Aliahidiwa nyumba na usafiri, haya yote hakuna ambalo TFF imelitekeleza kama mkataba wake unavyoelekeza,” kiliongeza chanzo chetu cha habari.

Watu wa karibu na kocha huyo, wamedai kuwa muda wowote baada ya mechi ya marudiano na Misri, atabwanga manyanga.

“Kama hatalipwa madai yake yote kufikia wakati huo, basi baada ya mechi dhidi ya Misri, Mkwasa ataachia ngazi,” walidai wapambe hao.

Stars inatarajia kurudiana na Misri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Juni 4. Katika mechi ya kwanza ugenini, Stars ilinyukwa mabao 3-0.

Jana gazeti hili liliwasiliana na Mkwasa kwa lengo la kutaka kujua ukweli wa madai hayo na alijibu kwa ufupi: “Suala la mkataba wangu na TFF ni siri, sipendi mambo yangu binafsi kuandikwa kwenye magazeti.”

Majibu ya Mkwasa yalikuwa ya mkato na hakutaka kufafanua kama kuna ukweli wowote na Nipashe ilipojaribu kumdadisi zaidi, alikata simu na hakupokea alipopigiwa tena.

Mtendaji Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alipoulizwa jana kuhusu suala hilo, hakuwa wazi kukubali au kukataa zaidi ya kusema: “Mkwasa ni mwajiriwa wa shirikisho, siwezi kutoa hadharani taarifa zinazomhusu.

"Siwezi kusema anadai au hatudai, hata mimi (Mwesigwa) au mwajiriwa mengine wa TFF, anaweza kuwa na madai yake, lakini taratibu haziniruhusu kusema."

Mwaka jana wakati akiagwa na wanahabari wa michezo, Rais Jakaya Kikwete ambaye katika utawala wake alichukua jukumu la kuwalipa makocha wa soka na michezo mingine, aliagiza makocha wazalendo walipwe kama ambavyo walikuwa wakilipwa makocha wa kigeni.

CHANZO: NIPASHE

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.