zanzibar

ZOEZI LA UCHUKUAJI FOMU ZFA LAZOROTA

UCHUKUAJI wa fomu za kuwania urais na Umakamu wa Rais ndani ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) umeanza kwa kusuasua, kwani ikiwa imeingia siku ya tatu tangu kutangazwa kuanza kuchukuliwa kwa fomu hizo, hakuna aliyejitokeza.

Akizungumza jana kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya ZFA, Kibabu Haji Hassan alisema hadi jana saa 7:00 mchana hakuna mgombea aliyejitokeza kuchukua fomu.

Alisema jana ilikuwa siku ya tatu tangu kutangazwa uchukuaji fomu, hakuna aliyejitokeza katika kituo cha Unguja, licha ya wengine kutangaza nia ya kuomba nafasi hizo.

Alisema uchukuaji fomu utasitishwa Aprili 6 mwaka huu, ambapo siku inayofuata kazi itakuwa ni kuzipitia fomu za wagombea.

“Mpaka muda huu naongea na wewe mwandishi sijapokea mgombea hata mmoja kuja kuchukua fomu na nadhani wanategeana, wapo waliotangaza nia lakini kwangu hawajaja kuchukua fomu,” alisema.

Uchaguzi wa ZFA Taifa unatarajiwa kufanyika Aprili 14 mwaka huu kisiwani Pemba, ambapo tayari kocha wa zamani wa JKU Salum Bausi na mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Simba kutoka Zanzibar, Abdul Mshangama wameshatangaza nia ya kugombea nafasi ya urais wakati Katibu wa zamani wa chama hicho, Mzee Zam Ali akitangaza kugombea nafasi ya Umakamu wa Rais kwa Unguja.

Fomu hizo za kuomba nafasi hizo kwa Unguja zinatolewa katika ofisi za chama hicho Amaan na kwa Pemba katika ofisi zake zilizopo Chake Chake.

Chanzo: Habari leo

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.