ICHUANO ya Mpira wa Kikapu ya Majiji inatarajiwa kufanyika Nairobi, Kenya mwaka huu, huku Dar es Salaam wakisema wamejipanga kwa mashindano hayo.
Nairobi ilipokea kijiti hicho kutoka kwa Tanzania iliyoandaa kwa misimu miwili ya mwaka juzi na mwaka jana, yote ikiwa Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili, Rais wa Chama cha Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), Mwenze Kabinda alisema wataendelea kufanya maandalizi ili kuwa na uwakilishi mzuri.
“Mwaka huu mashindano yanafanyika Nairobi, Kenya na tunatarajia kushiriki na kuendelea kutengeneza kiwango chetu, lengo ni kuhakikisha tunafanya vizuri ndani na nje,” alisema.
Kabinda alisema Dar es Salaam inakuwa na muunganiko wa wachezaji kutoka klabu mbalimbali, ambapo baadaye watatangazwa kwa ajili ya kuanza maandalizi.
Alisema uwezekano wa kufanya vyema upo kutokana na kwamba ndio kwanza wametoka kwenye mashindano ya mkoa, ambapo wachezaji wana nguvu na morali.
Msimu wa mwaka jana majiji ya Tanzania yaliyoshiriki michuano hiyo ni Tanga, Mbeya, Dar es Salaam na Mwanza.
Chanzo: Habari leo
0 comments:
Post a Comment