riadha

FABIAN AWA WATATU KUFUZU OLIMPIKI YA RIO

Fabian Joseph (wa pili kushoto mbele) akishiriki mbio za Dar Rotary mwaka jana jijini Dar es Salaam. Joseph ni i mmoja wa wanariadha waliofuzu kwa Olimpiki ya Rio 2016.
TANZANIA imekamilisha idadi ya wanariadha watatu watakaoshiriki mbio za marathoni katika Michezo ya 31 ya Olimpiki itakayofanyika Rio de Janeiro, Brazil baada ya Fabian Joseph kufuzu.

Awali wanariadha wawili tu wa Tanzania, Alphonce Felix na Said Makula ndio waliokuwa wamefuzu kwa michezo hiyo katika mbio za marathoni.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Francis John alithibitisha juzi kuwa, Joseph amefuzu baada ya Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) kuzitambua mbio za Hofu Marathoni zilizofanyika Japan, Desemba 20 mwaka jana.

Alisema Joseph alikimbia mbio hizo kwa kutumia saa 2:13.57, ambapo licha ya kuwa ndani ya muda wa kufuzu, lakini awali zilikuwa hazitambuliwi na IAAF hadi juzi walipotangaza kuzitambua.

John alisema sasa timu ya marathoni ya riadha itakayoshiriki Olimpiki imekamilika, lakini wanaweza kuibadili endapo watajitokeza wanariadha wengine watakaofanya vizuri zaidi katika mchezo huo.

Aidha, alisema Joseph ataondoka nchini Aprili 12 kwenda Japan kushiriki mbio za Marathoni za Magano zitakazofanyika Aprili 17,ambapo sasa atakwenda kwa ajili ya kuboresha muda wake badala ya kusaka viwango. Alisema jaribio la mwisho la wachezaji wa marathoni litafanyika Juni mwaka huu.

Chanzo: Habari leo

About Unknown

0 comments:

Powered by Blogger.