riadha

Mwanariadha wa Taifa avunja rekodi Ngorongoro

MWANARIADHA Ismail Juma jana alivunja rekodi ya njia ya mbio za Ngorongoro Marathon baada ya kumaliza wa kwanza kwa kutumia saa 1:02.48 na kuipiga teke ile ya awali ya saa 1:03.00 iliyowekwa miaka kadhaa iliyopita.

Tangu mwanzo wa mbio hizo jana zilizoanzishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, katika lango la kuingilia na kutokea Hifadhi ya Ngorongoro, Profesa Jumanne Maghembe, Juma alionekana kufanya vizuri kwa kuwatangulia wenzake kwa muda mrefu na kuwaacha mbali.

Baada ya kukimbia katika kundi moja na wenzake kwa karibu kilomita nne, Juma aliwaacha kuanzia hapo hadi mwisho wa mbio huku wenzake wakibaki wakisoma namba. Juma alimzidi mshindi wa pili kwa takribani dakika nne baada ya Stephen Uche kumaliza mbio hizo kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu akitumia saa 1:06.3 huku Yohana Elisante akishika nafasi ya tatu kwa saa 1:06.24.

Mwanariadha huyo ni miongoni mwa wanariadha wanaounda timu ya taifa inayotarajia kushiriki Michezo ya 31 ya Olimpiki itakayofanyika baadaye mwaka huu Rio, Brazil na atakimbia mbio za meta 5,000 na 10,000 endapo atafuzu.

Kwa upande wa wanawake, Fainuna Abdi ameendelea kuwaburuza wakongwe baada ya kuibuka wa kwanza katika mbio hizo kwa kutumia saa 1:11.52 na kumzidi mchezaji wa timu ya taifa Nathalia Elisante aliyemaliza wa pili kwa kutumia saa 1:15.46 huku Fadhila Tipa akiwa wa tatu kwa saa 1:16.54.

Kocha wa timu ya taifa ya Riadha inayojiandaa kwa Michezo ya Olimpiki iliyopiga kambi West Kilimanjaro mkoani Kilimanjaro, Francis John akizungumza kwa njia ya simu jana alisema Juma alistahili kushinda kwani yuko vizuri kutokana na mazoezi aliyofanya.

Naye Maghembe alisema anataka mbio za 10 za Ngorongoro ziwe za kimataifa zaidi na kutoa wanariadha watakashiriki na kushinda katika marathoni za kimataifa kama zile za London, New York, Boston na nyingine. Mbio hizo zimefanyika huku kukiwa na mvua kubwa iliyoanza kunyesha tangu juzi na kuendelea siku nzima ya jana.

Chanzo: Habari leo

About Unknown

0 comments:

Powered by Blogger.