kitaa

NAPE APINGA MAREKEBISHO YA KATIBA TFF

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema hakubaliani na marekebisho ya Katiba yanayotaka kufanywa na Shirikisho la soka Tanzania (TFF).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa hivi karibuni, alisema hakubaliani na mabadiliko hayo katika kipengele cha kupunguza idadi ya wajumbe watakaoipigia kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa shirikisho hilo.

Mwezi uliopita wajumbe wa TFF walikutana mjini Tanga kwenye mkutano mkuu ambapo walipewa marekebisho ya Katiba yakionesha moja ya mambo yanayopaswa kubadilishwa ni idadi ya wapiga kura kutoka wajumbe watatu kwenye kila chama na kuwa mmoja, lililopingwa na wajumbe wa mkutano huo.

Hata hivyo, Rais wa TFF Jamal Malinzi alisema watayaleta tena kwa wajumbe kwenye mkutano mkuu wa Desemba mwaka huu.

Alisema endapo TFF itaridhia mabadiliko hayo, ni dhahiri yataminya idadi ya wajumbe wanaowakilisha tasnia ya michezo nchini, ikiwemo kushindwa kushiriki kwenye maamuzi ya kimichezo nchini, ikiwemo kuwa na uwakilishi mdogo usioleta tija.

“Nimeona hili niliseme hapa Mwanza, hatuwezi leo kukubali kuminya idadi ya wapiga kura, mimi nadhani ni bora kuongeza idadi ya wapigakura kuliko kuwapunguza,” alisema.

Katika kuimarisha vyama vya michezo nchini ili kuvipa uhai, Nape alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vyema katika kuhakikisha vyama vinatekeleza majukumu yao kwa wakati, kubwa likiwa ni kuibua vipaji vya soka kwenye maeneo yao.

“Vyama visipoimarishwa vitakufa na badala yake watajipenyeza wajanja wachache kuingia kwenye vyama hivyo na watachaguliwa viongozi na baadaye wanaanza kupiga dili,” alisema.

Alisema Serikali itasimamia sekta ya michezo na kwamba haiko tayari kuruhusu uovu wowote kwenye sekta hiyo hususani mchezo wa soka unaopendwa na watu wengi.

“Serikali inachukua hatua ya kuviimarisha vyama vya michezo baada ya kugundua kuwa, baadhi ya vyama hivyo vilikuwa ni vya watu wajanja wachache ambao wengi wao wanaishi Dar es Salaam ambao hutengeneza mtandao wa kupanga safu za uongozi kwa kuwaweka madarakani viongozi wenye maslahi nao.“Tumegundua sekta ya michezo imevamiwa na wahuni wachache, na ndio maana tumeamua kuitoa Wizara sasa kutoka Dar es Salaam kuja mikoani, tunataka kuimarisha vyama vya michezo mikoani ili tuwapate viongozi makini na sahihi wanaokubalika kwenye sekta ya michezo,” alisema.

Alisisitiza kwa kusema; “Niwaombe Makatibu Tawala wa mikoa ambao ndio wenyeviti wa michezo wa mikoa watimize wajibu wao, watenge muda wa kukutana na vyama vya michezo ili wasimamie katiba za vyama hivyo.”

Chanzo: Habari leo

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.