Fainali za kuwania Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) sasa zitafanyika Juni 11, 2016.
Mchezo huo wa fainali utakaozikutanisha timu za soka ya Young Africans na Azam FC utafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema leo Mei 9, 2016 kuwa tarehe hiyo ni mwafaka kulingana na kalenda ya shughuli mbalimbali za soka.
“Ratiba inaonyesha hivyo,” amesema Malinzi alipozungumza ofisini TFF, Dar es Salaam.
Alichambua ratiba na kalenda hiyo kuwa Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kufikia kikomo Mei 21, 2016 kabla ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kuitwa kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’ unaotarajiwa kufanyika Mei 29, mwaka huu.
Taifa Stars itacheza mechi hiyo ikiwa ni maandalizi ya mchezo wake dhidi ya Misri unaotarajiwa kufanyika Juni 4, 2016 jijini Dar es Salaam kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Tayari TFF imefafanua iwapo Bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa msimu 2015/16 inayoendelea atashinda pia taji katika fainali za Kombe la Shirikisho la ASFC, ndiye atayeiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya mabingwa wa Afrika msimu wa 2016/17.
Kwa msingi huo, timu itayopoteza fungwa katika fainali hizo za Kombe la Shirikisho –ASFC linalodhaminiwa na kituo cha Televisheni cha Azam, ndiyo itakayowakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika katika msimu wa 2016/17
Fainali za Kombe la Shirikisho zinakuja baada ya mchuano ulioshindanisha timu 64 za Ligi Kuu Tanzania Bara - VPL (16); Ligi Daraja la Kwanza -FDL (24), Ligi Daraja la Pili – SDL (24).
0 comments:
Post a Comment