Wanariadha wa Zanzibar walioshiriki katika michuano ya riadha Afrika Mashariki chini ya miaka 20 |
Timu hiyo ilimaliza ikiwa ya sita katika mashindano hayo yaliyoshiriki mataifa 10 baada ya kuambulia medali moja ya dhahabu na moja ya fedha huku ikiondoka na medali tano za shaba.
Kocha wa timu hiyo, Robert Kalyahe alisema tatizo kubwa lililoigharimu timu yao ni muda mfupi wa mazoezi na uzoefu mdogo wa mashindano ya kimataifa.
Alisema kuwa timu hiyo ilikaa kambini wiki mbili tu Kibaha mkoani Pwani muda ambao ni mfupi kwani wengi wa wanariadha wake hawakuwa na mafunzo ya kutosha, hivyo walihitaji muda mwingi wa maandalizi.
Aidha, Kalyahe alisema kuwa wanariadha hao walihitaji muda mrefu wa maandalizi kwani walikuwa na mengi ya kujifunza ili kuwa fiti kwa mashindano hayo, ambayo Wakenya waliibuka washidi kwa kutwaa medali 13 za dhahabu, nane za fedha na nne za shaba.
Bingwa wa zamani wa dunia wa meta 1,500 Filbert Bayi alisema kuwa, tatizo kubwa la kufanya vibaya kwa timu hiyo ni kutokuwa na makocha wenye uwezo mkubwa wa kufundisha. Alisema makocha wetu wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi kuzungumza badala ya kufundisha wachezaji.
“Makocha wetu wengi wanatumia muda mwingi kuongea na sio kufundisha na hata uwezo wao ni mdogo,” alisema Bayi ambaye bado rekodi yake ya Jumuiya ya Madola haijavunjwa kwa zaidi ya miaka 40 sasa tangu aiweke.
Bayi aliweka rekodi ya dunia na mwaka 1974 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Christchurch, New Zealand. Rekodi yake ya dunia ilidumu kwa takribani miaka mitano ilipochukuliwa na Sebastiane Coe, ambaye sasa ni Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF).
Naye makamu mwenyekiti wa pili (Ufundi) wa Riadha Tanzania (RT), Dk Hamad Ndee alisema bila ya Serikali kuwekeza katika michezo kamwe hatuwezi kufanya vizuri katika michezo. Ndee ni muadhiri wa Idara ya Elimu kwa Michezo ya Shule ya Elimu ya Michezo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Chanzo: habari leo
0 comments:
Post a Comment