Licha ya kucheza kwenye kiwango bora na kuumiliki mpira dakika zote 90, Mbeya City fc imepoteza mchezo wake wa kujipima nguvu mbele ya Mtibwa Sugar ya Morogoro uliochezwa leo kwenye uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Kwenye mchezo huo ulioandaliwa na shirika la kidini la Faith Baptist, City iliuanza mchezo kwa kasi kubwa ikijenga mashambulizi kutoka eneo la katikati lililokuwa likiongozwa na Raphael Daud, ambapo Hemedy Murutabose aliyecheza mechi yake ya kwanza alishindwa kuipatia timu yake bao la mapema baada ya kuunganisha vibaya mpira uliokuwa umepigwa kutoka upande wa kulia na John Kabanda.
City iliendelea kulishambulia lango la Mtibwa kwa kasi, lakini umakini mdogo kwa washambuliaji Omary Ramadhan na Murutabose uliinyima City mabao ya mapema ambao kwa pamoja nyota hao wapya kikosini walikosa nafasi za wazi mara kadhaa ikiwemo ile ya dakika ya 30 ambapo Omary alishindwa kufunga akiwa yeye na golikipa wa Mtibwa na kuhitimisha dakika 45 za kwanza timu zote zikiwa hazijafungana.
Mtibwa walibadili mbinu kipindi cha pili na kufanikiwa kupata bao la kuongoza baada ya Rajab Zahir kuunawa mpira uliokuwa umepigwa na Rashid Mandawa na Henry Joseph kufanikiwa kufunga penati iliyotolewa na mwamuzi wa mchezo hii ilikuwa ni dakika ya 50 na dakika mbili baadae Haruna Chanongo alifunga bao la pili baada ya kuwatoka walinzi wa City.
Ramadhani Chombo aliifungia City bao hilo pekee lililohitimisha dakika 90 za mchezo huo na kuuacha ubao wa kusomea matokeo ukisomeka 2-1.
Mara baada ya mchezo kocha wa City Kinnah Phiri aliwasifu vijana wake kwa kuonyesha kandanda safi licha ya kupoteza mchezo.
“Tumekuwa bora kiwanjani siku ya leo, matokeo ni swala lingine, tulihitaji kuona ni jinsi gani tunaweza kucheza kutoka kwenye eneo letu kwenda kwa wapinzani wetu, hilo tumefanikiwa, hongereni kwa mchezo mzuri, yale yamepita kilichopo sasa tunakwenda kurekebisha makosa kadhaa tulioyaona kabla ya mchezo wetu mwingine hapo siku ya jumatatu dhidi ya Ruvu Shooting” alisema.
Chanzo: mbeyacityfc.com
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment