riadha

Nape mgeni rasmi uzinduzi Rock City Marathon

Msimu wa nane wa Rock City Marathon 2016 unatarajiwa kuzinduliwa Jumanne ya wiki ijayo jijini Dar es Salaam huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa ni Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye. Uzinduzi wa mbio hizo zinazoratibiwa na kampuni ya Capital Plus International utafuatiwa na uzinduzi mwingine utakaofanyika jijini Mwanza siku chache zijazo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa mbio hizo Bi Elizabeth Riziki alisema maandalizi ya mbio hizo kwa kiasi kikubwa yameshakamilika na zinatarajia kufanyika Septemba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza zikihusisha wanariadha kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo baadhi ya nchi za Afrika, Ulaya na Marekani.

Alisema mbio hizo zinazofanyika kwa mara ya nane mfululizo tangu zianze mwaka 2009 zina baraka zote kutoka Chama cha Riadha Tanzania (RT), pamoja na Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MRAA) kwa kuwa zinalenga kutambua na kuinua vipaji vya wanariadha nchini na pia kukuza utalii wa ndani kupitia sekta ya michezo. 

“Mbio hizi zimekuwa zikionyesha mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake, mafanikio ambayo kimsingi yamekuwa yakichagizwa na asili ya sehemu zinapofanyika. Jjiji la Mwanza limebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii na sisi kama waandaaji wa mbio hizi tumekuwa tukitumia fursa hiyo kuendelea kumulika vivutio vya kipekee vinavyopatikana katika ukanda wa ziwa Victoria,” alisema.

Alisema tayari baadhi ya makampuni yameshajitokeza kudhamini mbio hizo ikiwa ni pamoja na Freidkin Conservation Fund, African Wildlife Trust, Mwanza Hotel, Nyanza Bottlers Limited na kampuni ya Real PR Solution.

“Tunawaalika wadhamini waendelee kujitokeza kwa wingi ili kuzifanya mbio za mwaka huu kuwa bora zaidi,” alisema. Pamoja na Waziri Nape, uzinduzi huo unatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa michezo ikiwa ni pamoja na viongozi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), viongozi wa vyama vya riadha, wanariadha na wadau mbali mbali wa mchezo huo nchini.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.