judo

ZAIDI HAMIS: JUDO KUFANYA MAAJABU OLIMPIK

KOCHA wa timu ya taifa ya Judo, Zaidi Hamisi amesema kuwa, licha ya ugumu wa Michezo ya Olimpiki, mchezaji wake atafanya kitu katika michezo hiyo.

Michezo ya Olimpiki itafanyika kuanzia Agosti 5 hadi 21 Rio, Brazil na Tanzania inatarajia kupeleka wachezaji saba tu huku judo ikiwa na mwakilishi mmoja tena wa upendeleo.

Zaidi akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi juzi alisema kuwa, amefurahi sana kufanikiwa kupeleka mchezaji kwa mara ya kwanza katika michezo hiyo ya Olimpiki.

Kocha huyo ambaye yuko na timu hiyo mjini Moshi, ambako wamepiga kambi alikiri Olimpiki ni michezo migumu sana lakini alisema mchezaji wake ataweka historia kwa kufanya vizuri.

Alisema kuwa kwa miaka mingi Tanzania imeshindwa kupeleka mchezaji katika michezo hiyo lakini mwaka huu wameweza baada ya mchezaji huyo, Andrew Thomas kupata nafasi ya upendeleo.

Zaidi alisema kuwa nafasi hiyo ya upendeleo haijaja hivi hivi tu ila baada ya mchezaji wake kufanya vizuri katika mashindano tofauti yakiwemo yale ya Mataifa ya Afrika yaliyofanyika Brazzaville, Congo mwaka 2015.

Alisema mchezaji huyo pamoja na wengine watano wanajifua kinoma katika kambi yao mjini Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya michezo hiyo.

Alisema michezo hiyo ya Olimpiki itamsaidia mchezaji wake kujifunza kitu kutoka kwa wachezaji wenye uzoefu mkubwa ambao mara kwa mara wamekuwa wakishiriki michezo hiyo. Mbali na judo, Tanzania itapeleka timu ya kuogelea yenye wachezaji wawili wa upendeleo pamoja na wanne wa riadha akiwemo mwanamke mmoja.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.