vilabu

AFRICAN LYON : LENGO LETU KUBAKI VPL


UONGOZI wa klabu ya soka ya African Lyon umesema lengo lake kubwa ni kuhakikisha wanapigana kwa hali na mali ili kuibakiza timu yao kwenye Ligi Kuu.

Akizungumza na gazeti hili jana, kocha mkuu wa timu hiyo, Bernardo Tavares alisema timu yake msimu huu itapambana kuhakikisha inabakia katika ligi kuu kabla ya kuanza kupigania masuala mengine ikiwemo ubingwa.

"Tutahakikisha timu yetu inabaki Ligi Kuu na mkakati wetu mwingine ni kuhakikisha tunashinda kila mechi mbele yetu ili timu yetu imalize katika nafasi nzuri," alisema Tavares.

Kocha huyo wa zamani wa timu za vijana za Sporting Lisbon na Fc Porto za Ureno amewashangaa waamuzi jinsi wanavyochezesha mechi zao.

" Kiukweli waamuzi hawafanyi haki kabisa, mechi yetu na Azam tulistahili kushinda lakini mechi iliisha kwa sare ya 1-1 sijui yule mwamuzi alipewa rushwa," Tavares alisema.

African Lyon mpaka sasa imecheza mechi saba, imeshinda mechi moja, ikitoka sare mechi tatu na kupoteza mechi tatu huku ikiruhusu magoli ya kufungwa manane na kufunga magoli manne.

Tavares alisema kikosi chake hakina wachezaji wenye uzoefu, lakini kimejaa wachezaji wengi wenye umri kuanzia miaka 20 mpaka 22.

Kocha Tavares alisema kitu kingine alichogundua kuhusu soka la Tanzania kama timu sio Simba, Yanga au Azam inakuwa vigumu kushinda mechi.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa timu hiyo, Rahim Kangezi aliwaomba waamuzi wachezeshe kwa kufuata sheria za soka.

Chanzo : Habari leo

About dada

0 comments:

Powered by Blogger.