MUHTASARI WA MKATABA.
1. Bodi ya Wadhamini wa Young Africans Sports Club, (ambayo hapa inajulikana kama Mmiliki”) imeingia tarehe 3 September, 2016 Mkataba wa kukodishwa na kampuni ijulikanayo Yanga Yetu Limited (inayojulikana hapa kama “Mkodishwaji” kwa muhtasari wa maazimio yaliyoafikiwa katika Mkutano Mkuu wa Young Africans Sports Club uliofanyika tarehe 6 Agosti, 2016 ulitambua kuwa Young Africans Sports Club (anayejulikana hapa kama “YANGA”):
1.1 KWA KUWA, Timu ya Soka ya Mmiliki ni kongwe na yenye mafanikio kuliko timu ya soka nyingine zilizoko katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye thamani kubwa kiutamaduni na kwa urithi wa Taifa, licha ya jitihada zake zote, inakabiliwa na changamoto za kifedha katika kuiendesha timu yake ya mpira wa miguu, kwa kuwa na usajili mdogo wa uanachama, ukosefu wa mapato, ya ada za Wanachama, mifumo isiyo na ufanisi ya kiuendeshaji, kushindwa kujipatia kipato cha kibiashara kutoka katika hati miliki na nembo za kibiashara za Timu ya Soka ya YANGA kutoweza kujiendesha kibiashara na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Tanzania (TFF)- ambalo kwa mfululizo linasababisha YANGA kuiendesha Klabu yake kwa hasara na kuwa tegemezi kutoka kwa michango ya wahisani na kwa mikopo na kukabili changamoto hizi; na Mkutano wa Wanachama wa YANGA tarehe 6 Agosti 2016 uliazimia kugeuza hali hii kwa kukodisha Timu ya Soka ya YANGA ambayo ilikuwa inajiendesha kwa hasara na mapato madogo kupitia nembo yake na hakimiliki yake (jina na nembo) kwa muda wa Miaka (10), ili kuikinga Klabu kutoendelea kujiendesha kihasara katika kipindi cha Miaka (10) ya ukodishwaji, ijipange kiuwezo ili Timu ya Soka ya Mmiliki na hakimiliki za jina lake na nembo zitakapo rejeshwa baada ya kukodishwa kwa kipindi cha Miaka (10), YANGA itakuwa inaweza kujiendesha yenyewe na iwe na uwezo wa kifedha na iweze kushindana kikamilifu katika shughuli za mpira wa miguu.
2. Yanga Yetu Limited (inayojulikana hapa kama “Mkodishwaji”) ni Kampuni iliyoundwa ili iweze kuingia katika Mkataba na YANGA ili iweze kutimiza malengo ya Klabu kama yalivyo azimiwa katika Mkutano wa Wanachama wa YANGA uliofanyika tarehe 6 Agosti, 2016.
3. Baraza la Wadhamini wa Young Africans Sports Club baada ya mazungumzo na Mkodishwaji linapenda kuwafahamisha Wana YANGA kuhusu mambo muhimu yaliyomo kwenye Mkataba Huu ulioingiwa kwa kuzingatia na kwa haki miliki kutolewa kwa Mkodishwaji kwa njia ya Mkataba Huu, kwa kukodisha Timu ya Soka ya Mmiliki na haki zake zote, mamlaka na majukumu yote, jina lake na nembo kwa ajili ya kutumika kiamani na kibiashara katika kuziendesha shughuli za Timu ya Soka ya Mmiliki bila ya kuwa na kuingiliwa katika muda wa Mkataba huu kwa muda wa Miaka (10) kuanzia Tarehe ya Ufanisi ya 1 Septemba, 2016, ila kama utasitishwa kabla kufuatana na matakwa ya Mkataba:
3.1 Mkodishwaji atailipia YANGA deni la Shilingi bilioni kumi na moja na milioni mia sita na sabini na sita tu (Tshs. 11,676 billioni) inayodaiwa kama Mmiliki na Mkopeshaji mmoja.
3.2 Mkodishwaji atailipa YANGA Tshs 100 millioni kwa mwaka ambayo YANGA itawekeza kiwango kisichopungua (90%) ili kuimarisha mtandao wa Matawi yake.
3.3 Mkodishwaji atailipa YANGA katika mwaka wa fedha wowote ule kukiwa kuna faida ya fedha taslim ya asilimia 25% fedha ambayo YANGA itaitumia kujenga uwanja wake wa mpira.
3.4 Mkodishwaji atalipa hasara za uendeshadji zilizoko katika Mkataba kutoka kwenye mfuko wake bila ya kuweka madai kwa YANGA.
3.5 Mkodishwaji ataanza kuwekeza kwa vitega uchumi kuanzia siku (90) ya Mkataba katika mafunzo na vifaa, ambavyo kutakuwepo kiwanja cha mafunzo ya mpira katika sehemu atakayo ona inafaa kwake yeye Mkodishwaji.
3.6 Mkodishwaji atahakikisha kuwa majukumu yote ya kifedha ya Timu ya Soka ya YANGA ikijumlishwa ada ya usajili zinazotakiwa kuanzia Tarehe ya Ufanisi na majukumu mengine ya siku zijazo yanalipwa kulingana na mahitaji ya YANGA mapema kutoka kwenye mfuko wa Mkodishwaji.
3.7 Mkodishwaji atahakikisha kuwa Timu ya Soka ya YANGA haitamaliza chini ya nafasi nusu mwisho wa msimu wa ligi ya Tanzania Premium League wakati ikiwa ndani ya kipindi cha Mkataba.
3.8 Mkodishwaji atahakikisha kuwa Timu ya Soka ya Mmiliki iliyokodishwa katika kipindi cha misimu 3 mfululizo itamaliza ikiwa ni mshindi wa nafasi 2 za juu kwenye Tanzania Premium League.
3.9 Mkodishwaji, kwa kila mwaka atafadhili mashindano ya mpira katika mfumo utakao amuliwa na yeye Mkodishwaji kwa Timu ya Soka kwa vijana wenye umri chini ya miaka (18) na kila Tawi la Wanachama wa YANGA litaalikwa kutuma timu yake kushiriki katika shindano hilo.
3.10 Mkodishwaji atakabidhi kwa YANGA tuzo zozote au Nishani yoyote Timu ya Soka ya Mmiliki ikipata, na kuitaarifu YANGA kabla, pale itakapo wezekana, ili YANGA iweze kumteua mwakilishi wa kupokea tuzo hiyo kwa kuitambua Timu ya Soka ya Mmiliki.
3.11 Mkodishwaji ataingia katika Mikataba yote ya ufadhili au mikataba yaleseni kwa kuitisha zabuni kupitia Zabuni za Umma.
3.12 Mkodiswaji ataunda na kuiendesha Timu ya Mpira wa Miguu ya vijana kulingana na kanuni na miongozo ya TFF.
3.13 YANGA itateua moja kati ya kampuni Tano (5) za Ukaguzi Kongwe Duniani wa Mahesabu zije kukagua kwa kila mwaka hesabu za Mkodishwaji kuhakikisha hakuna ubadhirifu.
3.14 YANGA itakuwa na haki ya kipekee kabla ya Tarehe ya Ufanisi wa Mkataba huu kiwango chochote ambacho kinastahili kupata kutoka TFF, ikiwemo Mkataba wa Azam TV ambao unakadiriwa kuwa shilingi milioni mia tatu (300,000,000) kwa matangazo ya msimu uliopita, mikataba ya ufadhili, madeni ambayo haijalipwa, fedha za zawadi, VAT kutoka TFF na fedha zingine zote zitapewa umuhimu wa nafasi ya kwanza katika matumizi ya kukamilisha majukumu ya zamani ya Timu ya Soka ya YANGA ambayo yalijilimbikiza na hayakuwa wamelipwa.
3.15 Mkataba huu utakapo fikia ukomo, YANGA itakuwa na haki ya kurejesha kile ilichokikodisha.
4. Ilikubaliwa kwamba YANGA:
4.1 Itajitahidi mnamo kipindi cha miaka miwili ya Mkataba itakuwa na Wanachama hai 100,000 na kwa kila Wanachama 100,000 itateua Mjumbe mmoja kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya Mkodishwaji.
4.2 Itafanya kila juhudi ya kuongeza ardhi inayohitajika katika Makao Makuu yake yaliyopo mtaa wa Twiga ili iweze kujenga uwanja wa mpira unaofaa, ambao Mkodishwaji atawajibika kuchezea michezo yake ya Timu ya Soka ya YANGA, kwa masharti yatakayo kubaliwa baina ya Pande zote za Wahusika.
4.3 Itakuwa na haki katika wakati wowote ule ndani ya kipindi cha Mkataba kusitisha Mkataba ili mradi imfidie Mkodishwaji hasara zote za nyuma, ilipe malipo yote yaliyofanywa kwa YANGA na Mkodishwaji, inachukua mali zilizowekezwa na Mkodishwaji na kumfidia mapato ya siku zijazo – zote, hizi zikiwa zimetathminiwa na moja ya Kampuni za Wakaguzi (5) Kongwe Duniani.
4.4 Ikiwa Mkodishwaji atakarabati au atatumia mali yoyote ya YANGA ataifidia YANGA kwa masharti yaliyokubaliwa kwa masharti tofauti ya Mkataba Huu.
4.5 Mkodishwaji atakuwa na haki ya kipekee ya kiwakilishi (Exclusive Power of Attorney) kwa YANGA kufanya mikataba na TFF, CAF & FIFA kwa niaba ya YANGA bila ya kuingiliwa kati na YANGA lakini anapaswa atoe taarifa kuhusu uwakilishi huo kwa Baraza la wadhamini, kuanzia Tarehe ya Ufanisi wa Mkataba Huu pamoja na haki ya uwakilishi wa YANGA kwa: i) kuunda Kamati zinazohitajika na TFF, CAF na FIFA kuiendesha Timu ya Soka ya Mmiliki iliyokodishwa ii) kusajili au kulisimamisha benchi la ufundi na wachezaji kutoka Timu ya Soka ya YANGA, iii) Kuwa Msemaji Mkuu wa Timu ya Soka ya YANGA kwa Umma.
KUFUNGA.
5.1 Bodi ya Wadhamini wa YANGA inapenda kumshukuru Bw. Yusuf Mehbub Manji kwa kupendekeza masharti bora kuliko yale yaliyoazimiwa na kukubalika kwa Wanachama kwa manufaa ya YANGA, na tunampigia saluti uchangiaji wake usio na choyo kwa manufaa ya YANGA.
5.2 Tungependa kuufahamisha Umma kwamba Bw. Yusuf Mehbub Manji ametaka kujiuzulu kutoka Uenyekiti wa Klabu ili kuepusha mgongano wa kimaslahi, lakini tumelikataa ombi lake hili – kwa vile nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu, Wanachama wameonyesha kwa kura zao kuwa wana imani na uongozi wake, kwa vile wakati wa majadiliano, haweki maslahi yake binafsi juu ya yale ya Klabu, lakini anajaribu kadri iwezekanavyo kuisaidia Klabu kuweza kujitegemea kifedha haraka iwezekanavyo ili kuendelea kushindana katika mpira wa miguu kwa kiwango cha juu zaidi, hapohapo akilinda urithi wa Klabu na utamaduni – sifa ambayo tunaihitaji katika Mwenyekiti wa YANGA na kama akijiuzulu kutoka kwenye Klabu, tutakuwa tumempoteza kiongozi mwenye uzoefu na maadili ya hali ya juu wakati tunapofanya mageuzi ya YANGA.
Tunachukua fursa hii kuwafahamisha Wanachama na Mashabiki kuwa kuna kazi nyingi kwa faida ya YANGA ambazo Bw. Yusuf Manji anazifanya ambazo hazionekani mbele ya jamii: kitu ambacho kinahitajika katika Klabu. Tunapenda kuwafahamisha Wanachama na Mashabiki wawe waangalifu na maneno yao, kwa vile kauli za maneno ya matusi zinaumiza na zinawavunja moyo viongozi kama Bw. Yusuf Manji ambao tunafahamu hawagombei nafasi za Uongozi wa ndani ya Klabu, kwa sababu wanachukizwa na kutukanwa na Wanachama na hivyo basi, tunawapa mawaidha Wanachama, kwa manufaa ya Klabu watoe maoni yao kuhusu mambo ya soka na utawala wa soka, na siyo kwa watu na familia zao.
5.3 Sasa tunapenda kuwafahamisha Wanachama wa YANGA na Wapenzi wa YANGA kuwa kilichotiwa saini baina ya Pande Zote ni Mkataba ya kihistoria, na kama yakitekelezwa na pande zote mbili, YANGA itanufaika kwa hali ya juu mno kutokana na mazingatio na ushahidi iliyoupata kupitia Baraza lake la Wadhamini kwenye Mkataba wa ukodishwaji.
5.4 Mwisho, tumeombwa na Bw. Yusuf Manji tutangaze hadharani Mkataba Huu, hata hivyo bado tunajadiliana kama kutangazwa huko kutakuwa kwa manufaa ya Klabu, kwa kuwa, kwa upande mmoja ni vema kuwa na uwazi, lakini kwa upande mwingine washindani wa Klabu yetu wataiga Mkataba wetu kwa manufaa yao.
YANGA DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO
BODI YA WADHAMINI WA YANGA
0 comments:
Post a Comment