Kocha wa timu ya soka ya Taifa ya wanawake wenye umri wa chini ya miaka 20 (Tanzanite), Sebastian Nkoma, amekipongeza kikosi chake kwa kiwango walichokionyesha kwenye mechi dhidi ya Nigeria iliyofanyika Jumamoisu kwenye Uwanja wa Samuel Ogbemudian mjini hapa.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Nkoma, alisema kuwa kufungwa ni sehemu ya mchezo, lakini aliweka wazi vijana wake walipambana ila hawakuwa na bahati ya kupata matokeo waliyoyatarajia.
Kocha Nkoma alisema anaamini watafanya vizuri katika mechi ya marudiano itakayofanyika jijini Dar es Salaam huku akisema wana nafasi ndogo ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Mchezo wa marudiano utafanyika Oktoba mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam, uliko Chamazi, Dar es Salaam.
"Kazi haijamalizika, mmefanya kazi kubwa na mmewashangaza wote walioiangalia mechi hii, waliamini wangepata ushindi mnono zaidi ya huu, naamini tutafanya vyema katika mechi ya marudiano," alisema kocha huyo ambaye pia anafundisha timu ya wakubwa ya wanawake ‘Twiga Stars’.
Mkuu wa Msafara, Amina Karuma, alisema kuwa mapambano bado yanaendelea na anaamini kikosi chake kitashinda katika mechi ya marudiano itakayochezwa baada ya wiki mbili.
"Msife moyo wanangu, huu ndio mpira na unamatokeo ya aina tatu, naamini mtawashangaza tena tukia nyumbani," alisema Karuma ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Tanzania (TWFA) .
Aliongeza kuwa anashikuru wachezaji wote ni wazima na wataendelea na kambi ili kujiandaa na mchezo wa marudiano huku akiahidi kuwatafutia mechi ya kirafiki kabla ya kuwakaribisha Nigeria.
0 comments:
Post a Comment