kitaa

KUMWEMBE: NANGOJA FILAMU YA OKWI NA MAXIMO

Na Edo Kumwembe, Mwanaspoti

MARCIO Maximo. Alikuja nchini akiwa mtu wa kawaida. Baadaye kwa wajanja akageuka shujaa. Kwa wenye mtazamo wa karibu akageuka kuwa adui. Wakati anaondoka nchini akaonekana mjinga. Muda si mrefu pande zote mbili zikamuona alifaa. Nasikia anataka kurudi tena nchini kama shujaa.
Nasikia anakuja kujiunga na Yanga. Hakuna tatizo katika hilo. Yanga imara ndio Taifa Stars imara. Simba imara ndio Taifa Stars imara. Azam imara ndio Taifa Stars imara. Mbeya City imara ndio Taifa Stars imara.
Unaposikia kocha kama Maximo anakuja kufundisha timu kama Yanga hakuna unachoweza kufanya. unasubiri kwa hamu. Unalamba midomo kwa matamanio. Unajua tunaweza kuzalisha akina Jerry Tegete wengine. Akina Kiggi Makasi wengine.
Lakini upande wa pili wa kichwa unaanza kujiuliza maswali.
Waliomchukua Maximo wanamfahamu vizuri? Wanajua kwa nini alizalisha wachezaji kama akina Tegete? Jibu ni rahisi tu. Ni kwa sababu ya kiburi chake. Kiburi cha kuwaamini wachezaji chipukizi na msimamo wake wa kutoyumbishwa na wachezaji tunaowaona mastaa.
Kama Yanga wakiamini katika kiburi chake, Maximo atawafaa sana, hasa katika mechi za kimataifa na kuitengeneza timu imara ya kesho na keshokuwa. Kama Yanga hawataamini kiburi chake, basi hakuna walichofanya katika kumleta Maximo. Ni bora wangemwacha huko huko.
Mtu aliyemleta na kumlipa, Rais Jakaya Mrisho Kikwete alimwacha afanye kazi yake. Rais wa TFF iliyopita, Leodeger Tenga alimuacha afanye kazi yake. Swali linakuja kwa Yanga kama wanaweza kumwacha afanye kazi yake.
Kuna mfano mdogo tu wa mchezaji kama Emmanuel Okwi. Huyu ni staa sana katika soka letu. Lakini ameitumikia Yanga katika mechi chache sana tangu asajiliwe kwa uhamisho wa pesa mbaya kutoka Uganda.
Inadaiwa kuwa Okwi aligoma kucheza Yanga kwa sababu alikuwa hajalipwa pesa zake. Katika kesi kama hii, Maximo atakufa na viongozi wa Yanga kwa sababu hawezi kukubali kumkosa staa wake kwa sababu nyepesi kama hii.
Lakini kuna kesi ya pili. Wakati fulani Okwi anaweza kutimiziwa kila kitu na viongozi wake. Lakini bado anaweza kubaki nchini kwao kwa siku nyingi zaidi.
Hii sio kwa Okwi tu, bali hata kwa Hamis Kiiza ‘Diego’ na wachezaji wengi wengine wa kulipwa wa klabu mbalimbali nchini.
Viongozi watamwacha Maximo ashughulike nao wachezaji wa namna hii? Uamuzi wake wanaweza kuwa wa mwisho? Mara zote wachezaji wa namna hii wanachelewa, lakini unakuta viongozi wa klabu wanawapokea pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNI) kama Wafalme tena huku wakijigamba katika vyombo vya habari.

Wachezaji wetu hawana nidhamu kwa sababu wanamtumikia mtu aliyewasajili na hawamtumikii kocha wala klabu.
Mfumo huu haupo Taifa Stars na ilikuwa rahisi kwa Maximo kufanya kazi yake kwa sababu aliweka pamba masikioni.
Vinginevyo kama Yanga wakiishi vizuri na Maximo, kama atakuja, ana nafasi nzuri ya kuubadili mtazamo wa klabu kuhusu falsafa ya kuipeleka Yanga mbele.
Ni mzuri pia katika masuala ya utawala kama vile masuala ya udhamini, maandalizi ya mazoezi, mikataba ya wachezaji na mengineyo.
Itatetegemea Yanga wameongea nini na Mbrazil huyu. Kama waliongea kuhusu mshahara wake tu bila mengineyo, hapana shaka maisha yake Jangwani yanaweza yakajaa filamu nyingi za kusisimua.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.