TFF

TFF yaitaka lyon kufikisha mkataba wa Sounders

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeutaka uongozi wa klabu ya African Lyon kuwasilisha mkataba wake na Seattle Sounders ya Marekani kama wanataka kuendelea kuzitumia jezi zao katika Ligi Kuu.

Lyon ilikuwa ikitumia jezi zenye nembo ya Seattle Sounders FC ya Marekani jambo ambalo TFF imesema kuwa ni kinyume na kanuni na taratibu zinazoendesha ligi hiyo.

Akizungumza jijini jana Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema ili timu hiyo iweze kuendelea kuzitumia jezi hizo katika ligi inabidi ipelekee TFF mikataba yake inayoonyesha kuwa inadhaminiwa na Seattle Sounders.

“Ni kweli kabisa tunazo taarifa za timu hiyo kutumia jezi ambazo zina nembo ya timu moja ya Marekani katika baadhi ya mechi zake. “Hata hivyo uongozi wa timu hiyo uliwahi kutoa taarifa TFF juu ya kutumia jezi hizo, lakini tulitaka ufafanuzi wao na waonyeshe kuwa wanadhaminiwa na klabu hiyo jambo ambalo mpaka sasa hawajalifanya,” alisema Wambura.

Wakati huohuo; Uongozi wa Afrikan Lyon umesema uko katika mazungumzo ya mwisho na klabu ya Seatle Sounders ya nchini Marekani iliyojitolea kujenga uwanja pamoja na kituo cha michezo cha vijana hapa nchini.

Wamarekani hao ambao mbali na kutaka kuanzisha kituo hicho pia kila mwaka watakuwa wakichukua wachezaji watatu kwa ajili ya kwenda kuwafanyia majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini humo.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Sherraly Abdallah alisema tayari mazungumzo hayo yanaendelea chini ya mmiliki wa klabu ya African Lyon ambaye yupo nchini Marekani na mchakato wa kujenga kituo hicho unatarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.

Sherally alisema klabu hiyo ya Marekani hivi sasa wanaidhamini Lyon na wana mpango wa kujenga uwanja. Alisema makubaliano hayo yalifikiwa na viongozi wa pande zote mbili na kuahidi kuisaidia timu hiyo katika mahitaji mbalimbali.

"Ni kweli tayari mazungumzo yanaendelea kwa sasa na mmiliki wa timu Lyon yupo nchini Marekani, wamekubalia kutusaidia na sasa ndio wanaoisaidia timu yetu katika mambo mengi zikiwamo jezi na vitu vingine, watajenga kituo cha michezo ambacho kitakwenda sambamba na uwanja wa mpira ambao hautakuwa na tofauti sana na ule wa Azam,"alisema Sheraly.



mwananchi.co.tz

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.