Mchangani

TANZANIA WAPOTEZA KWA ZAMBIA SARPCCO

Timu ya mpira wa miguu ya Polisi Tanzania inayoshiriki michezo ya Umoja wa wakuu wa Polisi kwa nchi za kusini mwa Afrika (SARPCCO) imeanza vibaya baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya timu ngumu na bingwa mtetezi Polisi Zambia baada ya kukubali kichapo cha mabao 2 -1 katika  mchezo uliochezwa jana usiku katika uwanja wa taifa wa Namibia.
Mabao ya Zambia yalifungwa na mshambuliaji hatari wa timu hiyo Musukuma Chipunga katika dakika ya  15 na 20 baada ya uzembe uliofanywa na safu ya ulinzi wa timu ya Polisi Tanzania.
Bao la Tanzania lilipatikana kipindi cha pili kwa njia ya mkwaju wa penati baada ya kuangushwa kwa John Kanakamfumu katika eneo la hatari wakati akipokea pasi iliyopigwa na Saimon Lezire.
Penati hiyo iliwekwa kimiani na John Kanakamfumu baada ya kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa Zambia ambaye jana alikuwa mwiba kwa Polisi Tanzania baada ya kuokoa mashuti yaliyokuwa yakipigwa na wachezaji wa Tanzania.
Hata hivyo kipindi cha kwanza Polisi Tanzania haikucheza vizuri hadi kipindi cha pili baada ya kuingia kwa Delta Thomas, Madope Mwingira  na John Kanakamfumu ambao walionyesha uhai kwa timu ya Tanzania.
Katika Mechi nyingine ya kundi A, Polisi Zimbabwe ilishinda 2-1 dhidi ya Afrika kusini.
Wakati huohuo Wanariadha wameendelea kuipatia Tanzania Medali baada ya kuibuka mabingwa katika mbio za mita 5000, 1500 na washindi wa pili katika 5000 na kurusha tufe.
Waliopata medali jana ni pamoja na Fabian Nelson 5000 (Dhahabu), Basil John 1500 (Dhahabu), Wilbardo Peter 5000 (Fedha),Mohamed Ibrahimu  katika kurusha tufe (Fedha) na Basil John tena (Shaba) katika mbio za vijiti.
Mpaka sasa Polisi Tanzania ina medali tisa huku tatu zikiwa za Dhahabu,tatu  za fedha na tatu  za Shaba huku ikijiamini kupata medali nyingine katika michezo ya kurusha vishale (dats) mpira wa pete, mpira wa miguu na mbio za nyika.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.