Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kiingilio cha Sh 2,000 kwa mzunguko na Sh 5,000 kwa jukwaa kuu wakati timu ya taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 itakapocheza na Amajimbos ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Madagascar, mwakani.
Mchezo huo utaoanza saa 9.00 alasiri Jumapili Agosti 21, 2016 kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi – Mbagala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam utachezeshwa na Mwamuzi Noiret Jim Bacari wa Comoro akisaidiwa na Mmadi Faissoil na Said Omar Chebli wakati mezani atakuwa Ali Mohamed Adelaid huku Kamishna wa mchezo huo atatoka Somalia ambaye anaitwa Amir Abdi Hassan.
Jumamosi Agosti 6, 2016, Serengeti ilitoka sare ya 1-1 na Afrika Kusini katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Dobsonville ulioko Soweto, Mji ulioko Kusini – Magharibi mwa jiji la Johannesburg, mabao yote yalipatikana kipindi cha pili yakiwa ni ya penalti kwa kila upande. Afrika Kusini ndio walioanza kupata penalti katika dakika 65 iliyofungwa na Luke Gareth kabla ya Ally Msengi kuisawazishia Serengeti Boys katika dakika ya 70.
Penalti ya Afrika Kusini ilitokana na mmoja wa mabeki wa Serengeti Boys kumfanyia madhambi Linamandla Mchilizeli wa Amajimbos ndani ya eneo la hatari wakati ile ya Serengeti Boys ilitoakana na beki Luke Donn wa Amajimbos kunawa mpira eneo la hatari. Mwamuzi wa mchezo huo alikuwa, William Koto kutoka Lesotho.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime maarufu kama Mchawi Mweusi amesema: “Watanzania wakaribie Chamazi, waje kutushangilia ili tushangilie ushindi kwa pamoja kikosi change kiko vema na ninamshukuru Mungu kwa hilo, akili yangu na akili za wachezaji wangu ni kumuondoa Msauzi (Afrika Kusini).”
0 comments:
Post a Comment