TFF

NIGERIA KUTUA KESHO, KIINGILIO TSH500 AZAM COMPLEXS

Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu - wasichana wenye umri wa chini ya miaka 20 ya Nigeria ‘Falconets’ inatarajiwa kutua nchini usiku wa kumkia Ijumaa Septemba 29, mwaka huu.

Wakitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nnamdi Azikiwe, ulioko Abuja nchini Nigeria, Falconets watatumia ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia ikiwa ni kikosi cha watu 31 miongoni mwake wako maofisa 13 kuja Dar es Salaam, Tanzania. 

 

Timu hiyo ya wasichana yenye wachezaji 18, watatua Dar es Salaam saa 9.40 (03h40) usiku na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, limewapangia kuishi katika Hoteli ya Urban Rose iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam katika kipindi cha siku tatu watakazokuwa hapa jijini.

 

Wanakuja kucheza na timu ya Taifa ya wasichana wenye umri wa chini ya miaka 20 ya Tanzania ‘Tanzanite’ kwenye mchezo wa marudiano kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia. Fainali za Kombe la Dunia zitafanyika Ufaransa hapo mwakani.

 

Mchezo huo wa marudiano utafanyika Jumapili Oktoba mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10.00 jioni.

 

Tanzania ina matumaini ya kufanya vema kwenye mchezo huo wa marudio licha ya kupoteza kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Samwel Oigemudia ulioko Jimbo la Benin, Nigeria.

Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewapa fursa mashabiki wengi kuingia uwanjani kuishangilia timu ya taifa ya wanawake wenye umri wa chini ya miaka 20 ‘Tanzanite’ itakayocheza na Falconets ya Nigeria, Jumapili Oktoba mosi, mwaka huu.

TFF imetoa ofa katika kiingilio.

 

Kiingilio kitakuwa ni Sh. 500 tu kwa mashabiki watakaoketi eneo la mzunguko huku kwa wale watakaokaa Jukwaa Kuu (VIP) watalipia Sh. 1,000 tu katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.

 

“Lengo ni kuvutia mashabiki wengi wakaangalie soka la wanawake. Wakaingalie timu yetu. Wakaangalie uwezo wa timu yetu, waishangilie kwa nguvu zote,” amesema Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred.


Kocha wa Tanzanite, Sebastian Nkoma, amesema kwa namna alivyokiandaa kikosi chake ana imani kitaweza kupindua matokeo ya awali ambayo Tanzania kwa bahati mbaya ililala mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Samuel Ogbemudian, ulioko Jimbo la Benin nchini Nigeria, wiki mbili zilizopita.

About dada

0 comments:

Powered by Blogger.