Na Ezekiel Kitula
VIONGOZI wa timu ya Ruler’s New Power, aliyokuwa akiichezea Mtanzania, Douglas Didas Masaburi, aliyepata nafasi ya kucheza soka England, wamejitokeza na kudai wanataka wapewe haki yao.
Masaburi amepata dili la kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Coventry Spartans inayoshiriki Ligi Daraja la Pili England na wiki iliyopita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitangaza kuwa, Chama cha Soka cha England (FA), kimetuma maombi ya kutaka hati ya uhamisho ya mchezaji huyo.
Hata hivyo, TFF ilisema haiijui timu ya Ruler’s New Power anayotokea mchezaji huyo. Lakini viongozi wa timu hiyo, wiki iliyopita walitinga katika ofisi za Championi na kudai wanaishangaa TFF kusema haiwajui wakati wamesajiliwa kwa uhalali na Baraza la Michezo Tanzania (BMT).
Huku wakitoa kadi ya usajili wa timu yao, viongozi hao, Mwenyekiti, Everist Manembe na katibu wake, Said Mangunga, walidai wanachokitaka ni TFF kuwatambua na pia wapate haki zote zinazohitajika kutolewa ikiwa mchezaji huyo atauzwa.
“Sisi ni timu ya kukuza vipaji, tunapatikana maeneo ya Chanika (Dar es Salaam). Douglas (Masaburi) ni mchezaji wetu ambaye alikuwa na mkataba wa miaka miwili unaomalizika mwezi huu,” alisema Manembe huku akitoa kitambulisho cha mchezaji huyo.
“Hata jana (Alhamisi iliyopita) tulikuwa tukiwasiliana naye na alisema tufanye kila linalowezekana ili apate nafasi ya kucheza, hata wakati anaondoka Februari, mwaka huu alituaga. Leo (Ijumaa iliyopita) tunaandika barua TFF ili tupate haki yetu,” aliongeza.
Championi lilipoitafuta TFF kuzungumzia suala hilo, ofisa habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema: “Waje tuongee nao kama kweli ni mchezaji wao, maana hata sisi tunataka kuwajua. Hata kama mkataba wa mchezaji huyo unamalizika mwezi huu, kuna kitu watapata, kuna fidia ya mazoezi na vitu vingine kama hivyo.”
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment