
SIMBA, imeingia kwenye mzozo mwingine baada ya kutangaza kumsajili mchezaji wa Ashanti Shafii Hassan Rajab ambaye amesajiliwa pia na Zimamoto ya Zanzibar.
Mchezaji beki, alionekana juzi katika mazoezi ya Simba huku viongozi wa pande hizo mbili kila moja ikidai kumsajili kutoka Ashanti United ya Bara ambayo imeshuka daraja.
Akizungumzia usajili huo Katibu wa Zimamoto inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar Ali Jongo alisema kuwa mchezaji huyo ni wao na wamemsajili kutoka Ashanti na tayari wameshaingia naye mkataba wa miaka miwili.
“Sisi tunajua huyu ni mchezaji wetu na tunashangaa kumuona akifanya mazoezi na Simba wakati sisi tumeshamfungisha mkataba,” alisema Jongo.
Alisema, kutokana na hilo, wamepeleka taarifa kwa Chama cha soka Zanzibar (ZFA) ambao wamesema kuwa watafuatilia.
Rais wa ZFA Taifa Ravia Idarous Suleiman alikiri kupokea taarifa ya mdomo kuhusu hilo na wanasubiri vielelezo vyao ili wafuatilie zaidi.
“Sasa hivi siwezi kuzungumzia chochote kwani vielelezo havijaja bali tumepokea malalamiko kwa mdomo mara tu tukipata vielelezo tutawasiliana na wenzetu wa TFF ili kuona tunafanya nini katika kujuwa uhalali wa mchezaji huyu,” alisema Ravia.
Kwa upande wake Kocha Msaidizi wa Simba Selemani Matola alisema kuwa mchezaji huyo wamemsajili kutoka Ashanti na wao wameshamsainisha mkataba ingawa hakutaja ni wa muda gani.
“Sisi tumemsajili na kaanza rasmi mazoezi juzi usiku (Alhamisi) lakini kuhusu muda wa mkataba wake uongozi ndio unaojua,” alisema. Huu ni usajili wa pili wa Simba kuingia katika utata baada ya kumsajili Emannuel Okwi ambaye anamkataba na Yanga.
0 comments:
Post a Comment